SERIKALI imeajiri maofisa ugani 500 ili kuongeza uzalishaji wa korosho ghafi nchini kufikia tani laki 7 kwa mwaka 2025/2026 na tani Sh milioni 1 ifikapo mwaka 2029/2030.

Hayo yamejiri wakati wa uzinduzi wa mafunzo ya siku tano kwa maofisa hao waliyoajiriwa na Bodi ya Korosho Tanzania (CBT) chini ya programu ya Jenga Kesho iliyo Bora.

Lengo la mafunzo hayo yanayoendelea mkoani humo ni kuwajengea uelewa zaidi maofisa hao ugani namna ambavyo wanaenda kutekeleza majukumu hayo kwenye maeneo mbalimbali mkoani humo, yanayofanyika katika Manispaa ya Mtwara Mikindani. 

Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Mkuu wa Wilaya ya Mtwara Abdallah Mwaipaya alisema hatua hiyo ni utekelezaji wa vitendo wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi (CCM) chini ya Rais Samia Suluhu Hassan katika jitihada za kuendeleza zao hilo.

‘’Serikali yetu ni sikivu chini ya programu ya Jenga Kesho iliyo Bora, mumepata fursa hii ya kuaminiwa na kuwa sehemu ya wataalam mtakaoenda kuongeza ujuzi na kupata uzoefu wa ufikishaji wa huduma za ugani kwa wakulima ili waweze kuzalisha kwa tija zao la korosho na mazao mengine wanayolima,’’amesema Mwaipaya

Aidha, serikali imekuja na mpango huo ili vijana hao wakatekeleze shughuli za uendelezaji wa zao hilo ikiwemo kuhuisha kanzidata za wakulima wa korosho nchini, kusimamia usambazaji wa pembejeo, kutoa elimu ya matumizi sahihi na salama ya matumizi ya viuatilifu kwa wakulima hao.

Ameipongeza Cbt kwa usimamizi mzuri wa zao hilo nchini ambapo kwa mara ya kwanza katika msimu wa kilimo mwaka 2024/2025 wameshuhudia ongezeko la uzalishaji mkubwa wa korosho ghafi kutoka zaidi ya tani laki 300,000 msimu wa mwaka 2023/2024 hadi kufikia zaidi ya tani 400,000 msimu wa mwaka 2024/2025.

Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa CBT, Mangile Malegesi amesema maofisa ugani hao 500 waliyoajiriwa ni katika mikoa mitano ya asili inayolima korosho nchini.

Mikoa hiyo ikiwemo Mtwara, Lindi, Pwani, Ruvuma na Tanga ambapo kati ya hao mkoa wa mtwara wamechukuliwa 245 ambao ni takribani ya asilimia 60 ya maofisa kilimo wote waliyochukuliwa.

‘’Ajira yao ina lengo la kuwajengea ujuzi ili watambue fursa zilizopo kwenye zao la korosho na baada ya hapo waweze kupata ajira au kujiajiri wao wenyewe, kama tunavyotambua kilimo ndicho kilichotoa ajira nyingi nchini takribani asilimia 75 ya watanzani wako katika ajira za kilimo’’amesema Malegesi

Miongoni mwa washiriki wa mafunzo hayo akiwemo Shani Rajabu ameipongeza serikali kwa kuwapatia ajira na mafunzo kwa ujumla yatayosaidia kuwaongezea ujasiri na elimu wanayoenda kuwafikishia wakulima ili kuongeza tija.