Spika wa Bunge Dk Tulia Ackson(kulia0 akiwa na Mkurugenzi Mkuu wa NHIF Dk Irene Isaka.

Spika wa Bunge Dk Tulia Ackson ameupongeza Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) kwa maboresho makubwa yaliyofanyika hususan ya kuwafikia wananchi na kuwapa huduma bora.
Ameyasema hayo alipokutana na Menejimenti ya NHIF iliyoongozwa na Mkurugenzi Mkuu Dk Irene Isaka kwa lengo la kupata mrejesho wa huduma na namna mfuko ulivyojipanga kuwafikia wananchi hususan katika utekelezaji wa Bima ya Afya kwa Wote pamoja na huduma zinazotolewa na mfuko kwa Skimu ya Bima ya afya kwa Wabunge.
Dk Tulia amesisitiza umuhimu wa mfuko kuendelea kutatua changamoto zinazojitokeza na kuleta vikwazo kwa wananchi kujiunga na bima ya afya.

MKURUGENZI MKUU WA NHIF, DK IRENE ISAKA.
“Kwanza kabisa nikupongeze sana Mkurugenzi Mkuu kwa mabadiliko makubwa ya kihuduma uliyoyafanya kwa muda mfupi na kuwa na mafanikio yanayoonekana, niwasisitize tu muendelee kuangalia na kushughulikia changamoto zilizopo ili wananchi wasikwame kujiunga na huduma,” amesema Spika.
Akizungumzia maboresho yanayoendelea kufanyika ndani ya mfuko, Dk Isaka amesema kuwa kipaumebele cha mfuko ni kutumia mifumo ya TEHAMA ili kurahisisha usajili wa wanachama, ukusanyaji michango pamoja na uchakataji wa madai ili kuondoa malalamiko ambayo yamekuwa yakijitokeza mara kwa mara.
Aidha, ameeleza hatua iliyofikiwa na mfuko katika utekelezaji wa Bima ya Afya kwa Wote ambapo amesema tayari usajili wa makundi ikiwemo wanafunzi pamoja na watu binafsi umeanza kufanyika hivyo utoaji wa elimu unaendelea kuhakikisha kila mwananchi anajiunga na bima ya afya.
Amemhakikishia Spika kuwa, mfuko umeimarisha upatikanaji wa huduma bora za matibabu kwa wananchi nchini pamoja na kuwa na mfumo imara wa kujibu au kushughulikia changamoto zao kwa haraka.
Akizungumzia huduma zinazotolewa na NHIF kwa Bunge, Dk Isaka amesema mfuko umefanikiwa kuhudumia chombo hicho kwa muda wa miaka 10 hivyo akaahidi uboreshaji zaidi wa huduma kwa wabunge ili wawe na uhakika wa kupata huduma za matibabu kwao pamoja na wategemezi wao wakati wowote.