Umoja wa Mataifa umevitaja vita vya Sudan kuwa janga baya zaidi la kibinadamu duniani

Wanamgambo wa RSF nchini Sudan wanatuhumiwa kuvamia kambi kubwa ya wakimbizi ya Zamzam, kaskazini mwa Darfur.

Zamzam imekuwa ikilengwa katika vita vya Sudan vinavyoendelea tangu mwaka jana, lakini hii ni mara ya kwanza kwa RSF kuingia kambini humo.

Shambulizi hili la hivi punde ni sehemu ya juhudi za RSF kudhibiti miji ya karibu kama El Fasher, mji muhimu katikati ya vita vya Sudan, vinavyoingia mwaka wa pili.

Kwa mujibu wa wakimbizi wa ndani, wanamgambo wa RSF walivamia kambi hiyo Jumanne, wakiiba vitu na kuteketeza soko pamoja na makazi ya wakimbizi.

Khalid Drso, shahidi wa tukio hilo mwenye umri wa miaka 31, alisema kwamba tukio hilo lilikuwa la kutamausha, huku akiongeza kuwa hospitali inayohudumia majeruhi haina huduma za upasuaji.

Waziri wa Afya Kaskazini mwa Darfur, Ibrahim Abdullah Khater, alithibitisha kwa BBC kuwa majeruhi walizuiwa kuingia El Fasher kutokana na vizuizi vya RSF barabarani.

Hata hivyo, "Msemaji wa RSF alikanusha kuwa wapiganaji wa wao walishambulia kambi ya Zamzam, akisema walikuwa wakidhibiti kambi ya kijeshi iliyokuwa karibu na kambi ya wakimbizi.

Kambi ya Zamzam inahifadhi wakimbizi zaidi ya 500,000 waliohama makazi yao kwa hofu ya usalama wakati wa vita.

Mwaka jana, taasisi ya kimataifa inayohusiana na tathmini ya usalama wa chakula iliripoti hali ya ukame katika kambi hiyo, na janga la kibinadamu lilizidi kuongezeka baada ya shambulizi la RSF katika kambi hiyo.

Mashirika ya kimataifa ya misaada na madaktari walilaumu shambulizi hili, na mmoja wao alitaja kuwa mashambulizi kama haya yanachochea kushambuliwa kwa kambi za wakimbizi za Abu Shouk na Nefasha.

Shirika moja la kimataifa lisilo la kiserikali lilisema kuwa shambulizi hili linadhihirisha kwamba wakimbizi hawawezi kupata usalama, hata wanapojaribu kukimbilia maeneo ya kambi.