Polisi na waangalizi wa huduma ya afya wa serikali wanachunguza tukio hilo

Wauguzi wawili wa Australia wamesimamishwa kazi baada ya video kuonekana ikionyesha wakitishia kuwaua wagonjwa wa Kiyahudi na kujivunia kukataa kuwahudumia.

Mwanaume na mwanamke hao, ambao ni wafanyakazi wa hospitali moja mjini Sydney, sasa wanachunguzwa na polisi, kwa mujibu wa maafisa wa New South Wales (NSW).

Waziri wa Afya wa Jimbo la NSW, Ryan Park, alisema uchunguzi wa kina utafanyika ili kuhakikisha hakukuwa na madhara yoyote kwa wagonjwa, ingawa uchunguzi wa haraka wa rekodi za hospitali haukuonyesha kitu chochote kisicho cha kawaida.

Waziri Mkuu wa Australia, Anthony Albanese, alilaani video hiyo kama “ya kutisha na ya aibu” baada ya kuenea mtandaoni.

Hii inajiri chini ya wiki moja baada ya Australia kupitisha sheria kali dhidi ya uhalifu wa chuki kufuatia mfululizo wa mashambulizi makubwa ya chuki dhidi ya Wayahudi.

Video hiyo, ambayo BBC imeiona, inaonekana kurekodiwa hospitalini.

Mwanaume mmoja, ambaye anadai kuwa daktari, anamwambia Max Veifer kuwa “ana macho mazuri” lakini anaongeza “Pole wewe ni Mlowezi” kabla ya kusema kuwa anawatuma Wayahudi Jehanamu.

Anatengeneza ishara ya kukata koo, kisha mwanamke anakuja kwenye skrini na kusema kwamba “siku moja” bwana Veiffer “wakati wako utakuja” na utafa, na baadaye kuongeza kwamba hatamuhudumia Muisraeli. “sitawahudumia, nitawaua,” anasema mwanamke huyo.

Video hiyo imehaririwa, emojis zimeongezwa, na baadhi ya maoni yameondolewa - lakini mamlaka hazishuku ukweli wake.

Katika miezi ya hivi karibuni, katika matukio yasiyohusiana na video ya hospitali, kumekuwa na mashambulizi ya moto na uchoraji wa michoro inayohusiana na nyumba, magari, na sinagogi katika maeneo ya Kiyahudi kote Australia, jambo ambalo limezua hofu katika jamii.

Mkurugenzi Mtendaji wa Baraza la Utendaji la Wayahudi wa Australia, Alex Ryvchin, alisema video hiyo ni “ishara ya onyo tena kwa Wanaustralia wote kuhusu uovu unaoendelea katika jamii yetu.”