Bingwa wa zamani wa masumbwi, George Foreman.

BINGWA wa zamani wa uzito wa juu wa masumbwi duniani na mshindi wa medali ya dhahabu ya michezo ya Olimpiki wa Marekani, George Foreman amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 76.

Familia yake imetangaza habari za kifo cha shujaa huyo wa ndondi mapema leo.

Mwanamasumbwi huyo ameacha alama ya kipekee, ikiwa ni pamoja na pambano maarufu dhidi ya Muhammad Ali, linalojulikana kama “Rumble in the Jungle”.

Familia ya Foreman ikithibitisha kifo hicho kupitia mitandao yake ya kijamii imesema: “Mioyo yetu imevunjika. Kwa huzuni kubwa, tunatangaza kufariki cha mpendwa wetu George Edward Foreman Sr., ambaye ametutoka kwa amani, akiwa amezingirwa na wapendwa wake.”

Pigano la mwisho la Foreman lilikuwa mwaka 1997 likihitimisha kipindi chake cha kupigana kwa kuweka rekodi ya kushinda mara 76 na kupoteza mapigano 5.

Foreman amefunga ndoa mara nne kati ya miaka ya 1970 na 1980 lakini mwaka 1985 alifunga ndoa na Mary Joan Martelly alidumu naye hadi kifo chake.