BINGWA wa zamani wa kuogelea kutoka Zimbabwe aliyeshinda medali nyingi zaidi Afrika, Kirsty Coventry amechaguliwa kuwa Rais wa kwanza mwanamke wa Kamati ya Kimataifa ya Olimpiki (IOC) na pia, Mwafrika wa kwanza kushika wadhifa huo.
Kirsty mwenye umri wa miaka 41, aliwashinda wagombea sita, akiwemo Lord Sebastian Coe mshindi wa dhahabu mara mbili katika mbio za meta 1,500 na Rais wa Shirikisho la Riadha Duniani, pamoja na Juan Samaranch Jr Makamu wa Rais wa IOC.
Katika uchaguzi huo uliofanyika kwenye kikao cha 144 cha IOC huko Ugiriki, Kirsty alipata kura 49 kati ya 97 na kuwashinda, Juan Samaranch Jr aliyepata kura 28, Lord Coe kura nane na David Lappartient kutoka Ufaransa na Morinari Watanabe wa Japan kura nne kila mmoja.
Huku Prince al Hussein wa Jordan na Johan Eliasch wa Sweden wakipata kura mbili kila mmoja.
Akizungumza baada ya ushindi huo, Kirsty alisema kuchaguliwa kwake kama, Rais wa kwanza wa IOC na mwanamke Mwafrika kutasababisha ujumbe wenye nguvu juu ya usawa.
“Tumeweka alama kubwa, ni ishara kwamba kweli tupo kama taasisi ya kimataifa, tumekua na tutaendelea kukua huku tukijikita katika ufanisi na usawa kwa miaka ijayo,” alisema Kirsty.
Mwogeleaji huyo amewahi shinda medali saba kati ya nane ambazo Zimbabwe ilishinda kwenye Olimpiki, zikiwemo dhahabu mbili kwenye mashindano ya meta 200 ya kuogelea mtindo wa ‘backstroke’ katika michezo ya mwaka 2004 na 2008.
0 Comments