DODOMA: WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, George Simbachawene amemuagiza Katibu Mkuu, Utumishi, Juma Mkomi kuhakikisha kuwa barua za ajira kwa waliofaulu usaili zinatolewa katika mikoa husika walikofanyia usaili, badala ya kuwalazimu waajiriwa hao kusafiri hadi Dodoma kwenda kuzichukua katika Sekretarieti ya Ajira.

Akizungumza jijini Dodoma wakati wa uzinduzi wa Baraza la Wafanyakazi wa Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Waziri Simbachawene amesema kuwa utaratibu wa sasa unawasababishia gharama kubwa, usumbufu, na upotevu wa muda.

Ametoa mfano wa mtu aliyefanya usaili katika Mkoa wa Kigoma kulazimika kusafiri hadi Dodoma kufuata barua yake, kisha kurejea Kigoma au kwenda mkoa mwingine alikopangiwa, jambo ambalo amesema si haki kwa waajiriwa hao wapya.

“Hii si sawa, kwani tunawasumbua wanachoka hata kabla ya kuanza kazi. Tuwahurumie. Barua hizo wachukulie kwenye mikoa walikofanyia usaili. Tuwape dhamana makatibu tawala wetu, ambao tunaamini wana uwezo na maadili ya kutekeleza jukumu hilo,” amesisitiza Waziri Simbachawene.

Ameeleza kuwa anatamani kuona waajiriwa wapya wakichukua barua zao katika Ofisi ya Katibu Tawala wa Mkoa husika, badala ya kufanya safari isiyo ya lazima kwenda Dodoma kabla ya kuripoti vituo vyao vya kazi.