DODOMA: WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika maadhimisho ya Siku ya Nyuki Dunia yanayofanyika kuanzia leo uwanja wa Chinangali jijini Dodoma.

Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Dk Pindi Chana ametoa taarifa hiyo leo Mei 17, 2025 na kuongeza kuwa maadhimisho hayo ni uzingatiwaji wa Azimio la Bazara Kuu la Umoja wa Mataifa kutambua umuhimu na mchango wa nyuki katika maisha ya mwanadamu.

“Sote tunatambua kuwa nyuki na wadudu wengine wachavushaji wana mchango mkubwa sana katika usalama wa chakula, pamoja na uhifadhi bioanuwai na asilimia 80 ya mazao yote ya chakula hutegemea kuchavushwa na mdudu nyuki,” amesema Dk Chana.

SOMA ZAIDI: Mkutano mfugaji nyuki uwe fursa

Amesema pamoja na umuhimu wake bado nyuki yuko hatarini kutokana na shughuli za binadamu na kuwa maadhimisho ya mwaka huu yatapeleka ujumbe kwa Watanzania na dunia kuhusu umuhimu wa kumlinda nyuki na kutunza mazingira yake.

Maadhimisho ya mwaka huu yanabebwa na Kauli Mbiu ya ‘‘Nyuki kwa Uhai na Uchumi Imara, Tuwahifadhi’’ ambayo inaakisi maono na mwelekeo wa Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan.

Aidha, Dk Chana amesema maadhimisho haya yatafanyika sambamba na shughuli mbalimbali kwa siku nne maonesho, pia yatajumuosha matamasha ya nyuki mtaa kwa mtaa.

Pia kutakuwa na semina muhimu itakayohusu mnyororo wa thamani katika ufugani wa nyuki utakaongozwa na wataalamu wabobezi kutoka wizarani na wadau wa nje.

Dk Chana amesema pia kutakuwa na ziara ya mafunzo kwa wadau ambao watakwenda kwenye viwanda vinavyojihusisha na mazao yatokanayo na nyuki.

SOMA ZAIDI: Wanawake wahamasishwa ufugaji wa nyuki

Amesema wakati wote wa maonesho Tiba Nyuki itatolewa bure kwa wananchi watakaotembelea na kuhitaji huduma hii ambayo inasaidia kuimarisha kinga ya mwili.

“Katika eneo la maonesho kutakuwa na vivutio mbalimbali vya kitalii wakiwemo wanyamapori hai kama Simba, Tembo, Ndege Tausi na wanyama wengine.”

“Naomba kutoa rai kwa Watanzania wenzangu hususan wakazi wa jiji la Dodoma na mikoa ya jirani kuungana nasi katika kuadhimisha tukio hili muhimu kwa taifa letu,”