MTWARA: MWENGE wa Uhuru Kitaifa umepokelewa mkoani Mtwara ambapo utapitia miradi mbalimbali ya maendeleo 57 yenye thamani ya zaidi ya Sh bilioni 18.

Akitoa taarifa ya mapokezi ya mwenge huo leo Mei 17, 2025, Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Kanali Patrick Sawala amesema mwenge utakimbizwa katika halmashauri tisa mkoani humo.

Pia utakimbizwa kwenye njia yenye urefu wa kilomita 975.4 kuanzia Mei 17 hadi Mei 25 mwaka huu. Pamoja na shughuli nyingine, utaweka mawe ya msingi miradi 13 ya maendeleo.

Utafungua miradi minne, kuzindua miradi 13, kuona na kukagua miradi 27 inayotekelezwa na wananchi kwa kushirikiana na serikali kuu, wadau na halmashauri.

Mwenge huo umepokelewa katika kijiji cha Lumesule wilayani Nanyumbu mkoani mtwara ukitokea mkoani Ruvuma na utakabidhiwa mkoani Lindi Mei 26 mwaka huu katika kijiji cha Madangwa Halmashauri ya Wilaya ya Mtama kwenye mkoa huo.

SOMA ZAIDI:Mwenge wa Uhuru kuwashwa leo

Katika mkoa huo wa Mtwara, mwenge huo umeanza kukimbizwa wilayani Nanyumbu ambapo utapitia miradi mbalimbali 6 ya maendeleo ikiwemo ujenzi wa miundombinu ya maji, madarasa na mingine.

Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa mwaka 2025 zinaenda sambamba na kauli mbiu inayosema ‘Jitokeze Kushiriki Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025 kwa Amani na Utulivu’

“Mkoa wa Mtwara tunaendelea na utekelezaji wa ujumbe huu kwa vitendo, sasa tunaendelea kuhamasisha wananchi kujitokeza kushiriki katika uboreshaji wa taarifa zao kwenye daftari la kudumu la wapiga kura awamu ya pili,”amesema Sawala.