Mlipuko wa bomu nje ya kliniki ya uzazi ya California imeua mtu mmoja na kuwajeruhi wengine wanne katika "kitendo cha kukusudia cha kigaidi", maafisa wa FBI wamesema.

Mlipuko huo ulitokea kabla ya 11:00 saa za eneo chini ya maili moja kutoka katikati mwa jiji la Palm Springs, karibu na biashara kadhaa ikiwa ni pamoja na Vituo vya Uzazi vya Marekani (ARC). Kliniki hiyo ilisema hakuna mtu kutoka kituo hicho aliyejeruhiwa.

FBI baadaye ilisema ilikuwa na "mtu mmoja" anayefuatiliwa katika uchunguzi wake, lakini maafisa "hawakuwa wakimsaka" mshukiwa.

Michael Beaumier, shahidi, alisema aliangushwa na baiskeli yake na mlipuko huo. "Ulikuwa ni mlipuko mkubwa na nilisikia madirisha yakivunjika pande zote," alisema.

Rhino Williams, ambaye alikuwa katika mgahawa wake karibu, aliambia BBC awali alidhani mlipuko huo ulikuwa wa ndege au helikopta iliyoanguka.

FBI ilisema katika kikao kifupi cha Jumamosi kwamba lilikuwa shambulio la makusudi.

"Hiki kilikuwa kitendo cha kukusudia cha ugaidi. Uchunguzi wetu utakapoendelea tutabaini kama ni ugaidi wa kimataifa au ugaidi wa ndani," alisema Akil Davis, mkuu wa ofisi ya FBI ya Los Angeles.

Mkuu wa polisi wa Palm Springs Andy Mills alisema mlipuko huo uliharibu majengo kadhaa, mengine vibaya.

Aliongeza kuwa mtu aliyeuawa haijafahamika ni nani.