Watu wawili wamefariki na wengine 19 kujeruhiwa baada ya meli ndefu ya mafunzo ya Wanamaji wa Mexico kugonga Daraja la Brooklyn la New York City.
Polisi walisema Cuauhtémoc, ikiwa na watu 277, ilipoteza nguvu za umeme siku ya Jumamosi wakati nahodha alipokuwa akiendesha meli hiyo, na kuielekeza kwenye kingo za daraja upande wa Brooklyn.
Kanda za video zinaonyesha milingoti mirefu ya meli inakata daraja ilipokuwa ikipita chini ya muundo huo. Wafanyakazi walikuwa wamesimama kwenye nguzo huku wakiruka na kuanguka kwenye sitaha, mamlaka ilisema.
Mkazi wa Brooklyn, Nick Corso, aliyeshuhudia ajali hiyo, alisema ilisababisha hofu. Kulikuwa na "mayowe mengi, baadhi ya mabaharia wakining'inia kutoka kwenye milingoti," aliiambia AFP.
Meya wa jiji la New York Eric Adams alithibitisha kwenye mtandao wa X kwamba watu wawili walikufa na wawili kati ya 19 waliojeruhiwa walikuwa katika hali mbaya.
Daraja la Brooklyn halikupata uharibifu wowote na lilifunguliwa tena baada ya ukaguzi wa awali.
Polisi walisema wanaamini kuwa "maswala ya kiufundi" na kukatika kwa umeme ndiko kulikosababisha mgongano huo.
0 Comments