Papa Leo XIV ametawazwa na kuchukua rasmi majukumu yake ya upapa.

Akitoa hotuba yake, Papa aliweka vipaumbele vyake kwa upapa siku ya Jumapili, akikosoa unyanyasaji wa maskini na utawala wa kibabe wakati wa mahubiri kwa umati wa maelfu wakiwemo watu mashuhuri duniani.

Akizungumza katika uwanja wa St Peter's Square, Papa alitumia Misa yake kuangazia vipaumbele vya mtangulizi wake, Francis.

Alikosoa "chuki, vurugu, hofu ya utofauti na mtazamo wa kiuchumi ambao unatumia rasilimali za Dunia na kuwatenga maskini zaidi," alisema.

Makamu wa Rais wa Marekani JD Vance, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Marco Rubio na Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky walikuwa miongoni mwa waliohudhuria.

Vatican ilisema baadaye Papa atakutana na Zelensky kwa faragha ili kujadili vita nchini Ukraine.

Papa alisema alitaka kuona kanisa lenye umoja zaidi, na kwamba watu hawapaswi kujifungia katika vikundi vidogo na au kujiona bora zaidi ulimwenguni.

"Ninakuja kwenu kama kaka," alisema.

Katika mahubiri yake, papa wa 267 papa alisema atatafuta kutawala "bila kuingia katika majaribu ya kuwa mbabe".

Maelfu ya mahujaji walijaa uwanjani hapo na kusimama kwa heshima huku papa akipokea ishara za ofisi, kuwabariki watu na kutoa mwito mkali wa umoja.

Papa alipewa pete ya mvuvi na kadinali. Pete hii maalum ni ishara ya jukumu lake, na ni utamaduni wa tangu enzi za Mtakatifu Petro, ambaye alikuwa mvuvi.