SIMUYU: SERIKALI inakusudia kutoa kiwanja kwa ajili ya ujenzi wa ofisi za Chama cha Wafugaji Tanzania (CCWT) ili kurahisisha shughuli za wafugaji.

Hatua hiyo itasaidia kuratibu shughuli zote za mifugo ikiwemo utambuzi wa wafugaji kidigtali.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Ashatu Kijaji ametoa kauli hiyo leo Juni 14, wakati akijibu maombi ya wafugaji walioomba kupatiwa kiwanja kwa ajili ya ujenzi wa ofisi zao katika uwanja wa Kabindi Wilaya ya Bariadi, Simiyu.

Akizungumza na maelfu ya wafugaji, Waziri Kijaji amesema serikali Iko katika hatua za mwisho za kupata hati miliki kwa kuwasaidia wafugaji wote kupata ofisi itakayoratibu na kushughulikia malalamiko na changamoto.

SOMA ZAIDI

Akizungumzia mafanikio ya serikali ya awamu ya sita kwa wafugaji nchini Ashatu Kijaji amesema serikali imewezesha kutoa mbegu za malisho tani 105, kugawa madume kwa wafugaji 408 pamoja na ujenzi wa majosho 754 ndani ya miaka 4 ya utawala wa awamu ya 6.

Amesema kuwa serikali imeweka miundombinu kwa wawekezaji wa ndani ambao wanajenga viwanda vya kuchakata nyama na maziwa kwa kupunguza baadhi ya tozo ya kuingiza vifaa na hatua hiyo imechangia soko la kudumu kwa wafugaji ambao wanaongeza uchumi wa familia zao na taifa kwa ujumla.

Shughuli nyingine zilizofanywa na waziri ni kugawa vifaa vya kilimo kwa wafugaji ambao wanalima malisho ya mifugo yao pamoja na kuzindua television ya mifugo ambayo Itatoa maudhui yenye ujuzi wa kisasa wa kuwasaidia wafugaji kufuga kisasa.

Mwenyekiti wa Chama cha Wafugaji Tanzania (CCWT) Mrida Mshota amesema  mpaka sasa chama hicho kimesajili wafugaji 22,000 kidigtali na malengo ni kusajili wafugaji milioni nne ifikapo 2030.

Amemuomba waziri huyo kuhakikisha wafugaji wanapata usaidizi wa kuanzisha banki yao ya mifugo kwani zama za kufuga kimasikini zimeisha na sasa wafugaji wengi wanafuga kitajiri.

Ameishukuru Serikali kupitia Wizara ya Mifugo inavyorahisisha huduma za wafugaji ikiwemo wafugaji wengi nchini kupata fursa za kukopa mikopo ya kuendesha shughulikia zao bila Vikwazo ambapo chama hicho kimetoa tuzo maalumu kwa waziri wa mifugo kama waziri wa kwanza mwanamke anayeshughulikia maswala ya uvuvi na mifugo kwa ubunifu.