SHINYANGA: WAZEE wamekemea vitendo vya udhalilishaji vinavyofanyika kwenye mitandao ya kijamii huku wakisisitiza jamii kuendelea kudumisha mila na desturi zilizo nzuri na kuendeleza amani.

Mwenyekiti wa Baraza la Wazee Taifa, David Sendo amesema hayo leo Juni 14, 2025 kwenye Maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Kuelimisha na Kupinga Ukatili dhidi ya wazee yaliyofanyika mkoani Shinyanga yenye kauli mbiu ‘Wazee ni Hazina ya Taifa Tuwalinde Tuwatunze’.

Sendo amesema yapo mambo ambayo yanapaswa kufuatwa kama kuheshimu katiba ya nchi,,kudumisha upendo na ustahimilivu hivyo wazee wanapaswa kuheshimiwa kwani ni hazina na wameendelea kupinga vitendo vyote vya udhalilishaji nchini.

Aidha, ameonya baadhi ya waganga wa tiba za asili kutumia mwanya uchaguzi mkuu kutoa ramli chonganishi yatakayopelekea mauaji kwa wazee hivyo wasingependa yatokee mauaji ya aina yoyote kwa kipindi hiki.

Sendo amesema wazee waliomba vyama vya siasa hapa nchini vinavyoingia kwenye uchaguzi mkuu wahakikishe wanapitisha kwenye ilani zao changamoto za wazee ili kufikia matarajio yao lakini chama kimoja cha siasa ambacho ni Chama cha Mapinduzi (CCM) kilikubali maombi hayo na kuyafanyia kazi.

Sendo amesema pia walipeleka maombi hayo kwenye ofisi za Dira ya Taifa ya Maendeleo ya Jamii kwani kufanya hivyo kumetokana na kuathirika kwa muda mrefu kusubiri kupitishwa kwa sheria moja,sera ya wazee,haki na usalama ya wazee ,Wajibu wa baraza la wazee pamoja na kuboreshewa huduma na kutokomeza vitendo vya ukatili.

Mkuu wa wilaya ya Shinyanga, Julius Mtatiro akiongea kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Annamringi Macha amesema wazee waendelee kuwafundisha maadili vijana wao ili wanapoendelea kukua wasije wakawa wazee wasio kuwa na busara.

Mgeni rasmi katika Maadhimisho hayo Mwanaid Khamis amesema kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022 inaonyesha kuna wazee 3,406,6464 ambapo wanaume ni 1,546,221 na wanawake ni 1,860,243 sawa na asilimia sita.

Khamis amesema kundi hili limepata stahiki ili kuboresha ustawi na maendeleo yao ambapo kuanzia mwezi Julai 2024 hadi April 2025 wazee 4,975,473 wamepatiwa vitambulisho sawa na asilimia 27.65 na walithibitishwa na kupatiwa bima za afya za jamii zilizoboreshwa na madirisha zaidi ya 4,574 ya kutolewa huduma za afya yamewekwa kwa mikoa yote 26.

“Wizara hii iliundwa makusudi na kutengwa makundi maalum ili kujua kila eneo changamoto zenu hivyo Serikali inalijali kundi la wazee watumie vyombo vya dola kutoa taarifa za kikatili kwenye maeneo yao ambapo serikali imekuwa ikitoa huduma za afya wengine kupatiwa bure matibabu kwa wasiojiweza” alisema Khamis.

Khamis amesema zipo changangamoto zilizopo kwa wazee kutelekezewa na watoto wadogo wakati mwingine wamekuwa wakikutana na vitendo vya ukatili na kudhulumiwa haki zao ambapo matukio hayo yamefanywa na ndugu wakaribu kwenye familia zao.

Matukio ya ukatili yaliyo ripitiwa kwenye vituo vya polisi yameendelea kupungua ambapo mwaka 2022 yalikuwa matukio 130 ya mauaji,wanaume 29 na wanawake 101,mwaka 2023 matukio 152 wanaume ni 36 na wanawake ni 116 na mwaka 2024 yalikuwa matukio 138.