PWANISERIKALI ya awamu ya sita imekuwa ya vitendo kwa kukamilisha ujenzi wa Hospitali ya Halmashauri ya Mji Kibaha mkoani Pwani kwa kutoa fedha Sh bilioni 4.19 kukamilisha ujenzi huo.

Hayo yamesemwa na Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake (UWT) wa Chama Cha Mapinduzi Taifa (CCM, Mary Pius Chatanda leo Juni 15,2025 akiwa kwenye ziara ya kikazi ya kukagua Utekelezaji wa Ilani ya CCM 2020/2025 na Kutoa Elimu kwa Wananchi juu Ilani Mpya ya 2025/2030 mkoani Pwani.

Akiwa wilayani humo Chatanda amesema fedha hizo zimejenga majengo, miundombinu mbalimbali pamoja na ununuzi wa vifaa tiba lengo ni kuboresha sekta ya afya katika kila wilaya nchini.

Imeelezwa kuwa hadi sasa wastani wa wananchi 247,110 wanapata huduma kutoka kwenye hospitali hiyo na kuimarisha huduma za rufaa, huduma za kibingwa za mama na mtoto ambazo zilikuwa hazipatikani hapo awali.

Hospitali hiyo ya Halmashauri ya Mji wa Kibaha imesaidia kuboresha huduma za afya kwa wananchi na sasa wanapata huduma za matibabu kwa ukaribu bila kulazimika kusafiri umbali mrefu na imepunguza idadi ya Vifo vinavyoweza kuzuilika.

Katika ziara hiyo Chatanda alitembelea mradi wa soko la kisasa ‘Kibaha Shopping Mall’ ulitekelezwa na serikali kupitia Halmashauri ya Mji Kibaha ambao utekelezaji wake ulioanza mwaka 2028 na kukamilika 2019 katika Eneo la Kitovu Cha Mji (CBD) kwa Fedha za Serikali Kuu, (UNCDF) na Mapato ya Ndani na kufanya jumla ya Mradi wote hadi kukamilika umetumia Sh bilioni 8.35.