Rais William Ruto amejaribu kuwatuliza wakenya kuhusu mpango huo

Mahakama ya Kenya imesitisha utekelezwaji wa mpango wa msaada wa afya wa $2.5bn (£1.9bn) uliotiwa saini na Marekani wiki iliyopita kutokana na masuala ya faragha za data.

Ni kesi iliyowasilishwa na kikundi cha kutetea haki za watumiaji kutaka kukomeshwa kuhamisha data binafsi za Wakenya chini ya makubaliano hayo.

Uamuzi huo wa muda sasa unaIzuia Kenya kuchukua hatua zozote za kutekeleza mpango huo.

Tangu makubaliano hayo na Kenya, utawala wa Donald Trump umetia saini makubaliano kama hayo na mataifa mengine ya Afrika huku akifanyia marekebisho mpango wake wa misaada ya kigeni.

Chini ya mkakati wake mpya wa misaada ya afya duniani, Marekani inatoa kipaumbele mikataba ya moja kwa moja na serikali badala ya kutoa ufadhili kupitia mashirika ya misaada.

Nchi zinahitajika kuongeza matumizi yao katika taasisi za afya. Katika mpango huu na Kenya, Marekani ingechangia dola bilioni 1.7, huku serikali ya Kenya ikichangia dola milioni 850.

Katika sherehe ya utiaji saini wiki iliyopita, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Marco Rubio aliuelezea kama "mkataba muhimu".

Tangu wakati huo Marekani imeingia katika mikataba kama hiyo na Rwanda, Lesotho, Liberia na Uganda.

Hata hivyo, Wakenya wengi wameibua wasiwasi kwamba mpango huo unaweza kuruhusu Marekani kutazama rekodi binafsi za matibabu kama vile hali ya VVU, historia ya matibabu ya TB na data juu ya chanjo.

Mahakama Kuu ilikubali kuzuia kutekelezwa kwa mpango huo hadi kesi kamili isikilizwe.

Serikali ya Kenya imejaribu kuwatuliza raia kuhusu mpango huo.

Siku ya Jumatano, Rais William Ruto alisema mwanasheria mkuu alipitia makubaliano ili kuhakikisha kuwa "sheria inayotumika kuhusu data ni sheria ya Kenya."

Marekani haijatoa maoni yoyote kuhusu masuala faragha.

Kesi hiyo itatajwa tena Februari 12.