Nahodha wa Ureno Cristiano Ronaldo amesema hatastaafu kucheza soka hadi atakapofunga bao lake la 1,000.
Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 40 alifunga mabao mawili katika ushindi wa Al-Nassr wa 3-0 dhidi ya Al Akhdoud siku ya Jumamosi na kufikisha jumla ya mabao 956 aliyofunga kwa klabu na timu ya taifa.
Mshambuliaji huyo, ambaye alijiunga na Al-Nassr 2022, alisaini mkataba mpya wa miaka miwili na klabu hiyo ya Saudi Arabia Julai iliyopita ambao unampeleka zaidi ya siku yake ya kuzaliwa ya kutimiza miaka 42.
Akizungumza baada ya kutajwa kuwa Mchezaji Bora wa Mashariki ya Kati katika Tuzo za Soka za Globe huko Dubai siku ya Jumapili, Ronaldo alisema: "Ni vigumu kuendelea kucheza, lakini nina motisha."
"Shauku yangu ni kubwa na ninataka kuendelea. Haijalishi nacheza wapi, iwe Mashariki ya Kati au Ulaya. Nafurahia kucheza mpira kila wakati na nataka kuendelea."
"Mnajua lengo langu ni nini. Nataka kushinda mataji na nataka kufikia idadi hiyo [mabao 1,000]. Nitafikia idadi hiyo bila shaka, ikiwa sitopata majeraha."
Katika mahojiano na Piers Morgan mwezi uliopita, Ronaldo alisema anapanga kustaafu soka "hivi karibuni."
Ronaldo amefunga mabao 13 katika mechi 14 msimu huu akiwa na Al-Nassr, na wako mbele kwa pointi nne kileleni mwa jedwali katika Ligi ya Saudi Pro.
Ronaldo anashikilia rekodi ya kufunga mabao mengi zaidi kwa Ureno (143) na Real Madrid (450), na ndiye mchezaji pekee aliyefunga mabao zaidi ya 100 kwa vilabu vinne - Manchester United, Real Madrid, Juventus na Al-Nassr.
Mshambuliaji huyo alisema mwezi Novemba kwamba Kombe la Dunia la 2026 nchini Marekani, Canada na Mexico litakuwa mashindano yake ya mwisho ya kimataifa.
Alikuwa nahodha wa Ureno waliposhinda Euro 2016 nchini Ufaransa.

0 Comments