Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu amesafiri kwenda Florida kukutana na Rais wa Marekani Donald Trump. Netanyahu anatarajiwa kufanya mikutano tofauti leo, Jumatatu, na Rais Trump pamoja na Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Marco Rubio.
Hatima ya Ukanda wa Gaza na mpango wa makombora ya Iran ni miongoni mwa mambo muhimu yatakayojadiliwa katika mazungumzo kati ya Netanyahu na Donald Trump.
Hali ya usalama nchini Lebanon pamoja na suala la kunyang’anywa silaha kwa kundi la Hezbollah pia ni masuala muhimu katika ajenda ya mazungumzo hayo.
Hii ni ziara ya tano ya Waziri Mkuu wa Israel nchini Marekani tangu aliporejea madarakani. Mkutano huu kati ya viongozi wa Marekani na Israel unafanyika wakati ambapo kipaumbele cha Rais Trump ni kutangaza utekelezaji wa awamu ya pili ya mpango wa amani wa Gaza unaotarajiwa kuanza mwezi ujao, huku Benjamin Netanyahu akisisitiza zaidi kuzingatia kile anachokiita “tishio la Iran.”
Awamu ya kwanza ya mpango huo, uliokubaliwa mwezi Oktoba, ilijumuisha kusitisha mapigano, kuondolewa kwa sehemu kwa wanajeshi wa Israel kutoka Ukanda wa Gaza, pamoja na kuwasilishwa kwa misaada ya kibinadamu.
Awamu ya pili inajumuisha kuundwa kwa serikali ya kitaalamu katika Ukanda wa Gaza, kupelekwa kwa kikosi cha kimataifa cha kuimarisha usalama, pamoja na kunyang’anywa silaha taratibu kwa Hamas.
Serikali ya Israel inasisitiza kuwa ujenzi upya wa Gaza haupaswi kuanza hadi Hamas itakaponyang’anywa silaha kikamilifu na mateka wote kuachiliwa.
Hamas tayari imerudisha mateka au mabaki yao, lakini bado haijarudisha mwili wa Sajenti Ron Gweli nchini Israel. Baraza la usalama la Israel pia limekataa kufungua kikamilifu mpaka wa Rafah.

0 Comments