Donald Trump amesema anatumai awamu ya pili ya mpango wa amani wa Gaza itafikiwa "haraka sana," huku akiionya Hamas "itaingia matatizoni" ikiwa haitoweka silaha chini haraka.
Rais wa Marekani, ambaye mpango wake wa amani wa vipendele 20 unalitaka kundi hilo kweka silaha chini, alitoa kauli hiyo alipokutana na Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu huko Florida kwa mazungumzo siku ya Jumatatu.
Wakati wa mkutano na waandishi wa habari na Netanyahu baada ya mkutano wao, Trump alisema Israel "imetimiza mpango huo kwa asilimia 100," licha ya jeshi lake kufanya mashambulizi huko Gaza.
Rais wa Marekani pia amesema nchi yake inaweza kuunga mkono shambulio jingine kubwa dhidi ya Iran iwapo itaendelea kujenga upya makombora ya masafa marefu au silaha za nyuklia.
Alipoulizwa ni kwa jinsi gani Hamas na Israel zitaingia katika awamu ya pili ya mpango wa amani, Trump alisema: "Lazima kwanza waweke silaha chini."
Akiizungumzia Hamas, amesema: "Kama hawataweka silaha chini kama walivyokubali, wataingia matatizoni."
"Wanapaswa kuweka silaha chini ndani ya muda mfupi sana".
Trump pia amesema ujenzi mpya huko Gaza unaweza "kuanza hivi karibuni."
Mpango wa amani wa Gaza ulianza mwezi Oktoba. Katika awamu ya pili, serikali ya wasomi itaanzishwa katika eneo hilo, Hamas itaweka silaha chini na wanajeshi wa Israel wataondoka. Ujenzi mpya wa Gaza utaanza.
Lakini wakosoaji wanasema Netanyahu anaweza kutaka kuahirisha mchakato huo na badala yake kuishinikiza Hamas kuweka silaha chini kabla ya wanajeshi wa Israel kuondoka.
Waziri mkuu wa Israel ameshutumiwa kwa kutotaka kuzungumzia suala la mustakabali wa kisiasa wa Palestina.
Maafisa wa Hamas wamesema upokonyaji silaha unapaswa kufanyika sambamba na maendeleo ya kuelekea taifa huru la Palestina.
Tangu kuanza makubaliano ya kusitisha mapigano, Wapalestina 414 wameuawa na jeshi la Israeli huko Gaza, kulingana na wizara ya afya inayoongozwa na Hamas.
Wakati wa mkutano na waandishi wa habari, Trump pia alionya kwamba Marekani itaanzisha mashambulizi zaidi dhidi ya Iran ikiwa itabainika kutengeneza silaha za nyuklia.
Mazungumzo ya Trump na Netanyahu pia yalilenga katika maeneo mengine ya mvutano wa kikanda, ikiwa ni pamoja na Syria na kundi la wanamgambo wa Hezbollah nchini Lebanon.

0 Comments