Rais Volodymyr Zelensky amekanusha madai ya Urusi kwamba Ukraine imefanya shambulio la ndege zisizo na rubani kwenye moja ya makazi ya Rais Vladimir Putin, na kuishutumu Moscow kwa kujaribu kuvuruga mazungumzo ya amani.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Urusi Sergei Lavrov anadai Kyiv ilifanya shambulio usiku kwa kutumia ndege 91 zisizo na rubani (UAVs) kwenye makazi ya Putin katika eneo la kaskazini magharibi mwa Novgorod nchini Urusi.

Urusi imesema sasa itapitia upya msimamo wake katika mazungumzo ya amani. Bado haijabainika Putin alikuwa wapi wakati wa shambulio hilo.

Zelensky amekanusha madai hayo akisema ni "uongo wa Urusi," uliokusudiwa kuipa Kremlin kisingizio cha kuendelea na mashambulizi dhidi ya Ukraine.

Amesema Urusi imewahi kushambulia majengo ya serikali huko Kyiv.

Zelensky alisema kwenye X: "Ni muhimu dunia isikae kimya sasa. Hatuwezi kuruhusu Urusi kudhoofisha juhudi za kufikia amani ya kudumu."

Katika taarifa aliyoichapisha kwenye Telegram siku ya Jumatatu, Lavrov alisema ndege zote zisizo na rubani 91 alizodai zilirushwa kuelekea nyumbani kwa Putin zilizuiwa na kuharibiwa na mifumo ya ulinzi wa anga ya Urusi.

Aliongeza kuwa hakukuwa na ripoti za majeruhi au uharibifu kutokana na shambulio hilo.

"Kwa kuongezeka jinai za utawala wa Kyiv, ambao umebadilika na kuwa na sera ya ugaidi wa serikali, msimamo wa Urusi katika mazungumzo ya kusaka amani utapitiwa upya," alisema.

Lakini aliongeza kwamba Urusi haina na nia ya kujiondoa katika mchakato wa mazungumzo na Marekani, shirika la habari la Urusi Tass liliripoti.

Madai hayo ya Moscow yanakuja baada ya mazungumzo kati ya Marekani na Ukraine huko Florida siku ya Jumapili, ambapo Marais Trump na Zelensky walijadili mpango mpya wa amani wa kukomesha vita.

Baada ya mkutano huo, Zelensky aliambia Fox News Jumatatu kwamba kuna "uwezekano wa kumaliza vita hivi" mwaka 2026.

Lakini alisema Ukraine haiwezi kushinda vita bila msaada wa Marekani.