
CHAMA cha Alliance for Change and Transparency (ACT Wazalendo) kimesema kushiriki katika Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar (SUK) si kipaumbele chake kwa sasa.
Kimesema kwa sasa kinajikita kuhakikisha kinajenga uelewa kwa Wazanzibari kutambua misingi na malengo ya uwepo wa umoja huo.
Makamu Mwenyekiti wa ACT Wazalendo Bara, Isihaka Mchinjita alieleza hayo Dar es Salaam wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu maazimio ya kikao cha Kamati Kuu ya ACT Wazalendo kilichofanyika Januari 18, 2026.
“Kwa sasa kipaumbele cha ACT Wazalendo ni kuona namna gani malengo ya kuundwa kwa serikali hiyo yanafanyiwa kazi. “Hatuwezi kujadili kama tunaweza ingia au kutoingia bila kujadili misingi yenyewe ya Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK) kama inafuatwa kwa sababu ili serikali hiyo iwe halali lazima itanguliwe na uchaguzi wa uwazi na haki kwa hiyo lazima tushughulike na hilo kwanza kabla ya kuingia,” alisema.
Alieleza miongoni mwa malengo ya kuundwa kwa SUK ni kuwa chombo cha kuwaunganisha Wazanzibari pamoja ili kutatua changamoto zao za ndani na kuongoza nchi yao katika namna ambayo itawaweka pamoja.
Alisema pia chama hicho kinatarajia kuifungulia kesi Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) kwa sababu kwa mujibu wa sheria hadi sasa tume hiyo ilipaswa iwe imechapisha kwenye gazeti la serikali matokeo ya Uchaguzi Mkuu wa 2025 lakini hadi siku hizo zimepita bila matokeo hayo kuchapishwa.
“Tunakwenda mahakamani ili kuwaambia walete matokeo hayo na tunaamini tukifika mahakamani tunaweza kuainisha upungufu wote ulioonekana kwenye uchaguzi mkuu,” alisema.
Mchinjita alieleza Kamati Kuu imeazimia ACT Wazalendo itaongoza mapambano ya kupigania mchakato wa Katiba mpya kwa sababu bila Katiba mpya hakuna demokrasia na haki.
Alieleza ili kufanikisha hilo watahakikisha serikali inapitia upya na kufanyiwa marekebisho kwa sheria ya mabadiliko ya katiba na sheria ya kura ya maoni ili kukidhi matakwa ya sasa na kuhuisha mchakato wa Katiba mpya.
0 Comments