
ZIWA Victoria linaendelea kurejea katika nafasi yake kama nguzo kuu ya mfumo wa usafiri na biashara nchini
Tanzania. Hii inatokana na uwekezaji mkubwa unaofanyika katika miundombinu ya bandari, usafiri wa majini na uunganishaji wa reli.
Kupitia hatua zilizoratibiwa na Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) Tanzania inaliweka upya ziwa hilo kubwa zaidi barani Afrika kuwa korido muhimu ya kimkakati ya usafirishaji wa mizigo na abiria likihudumia eneo la Maziwa Makuu na kukamilisha mitandao ya kitaifa ya usafiri.
Ziwa Victoria ambalo ndilo ziwa kubwa zaidi lenye maji safi Afrika, linaunganisha Tanzania moja kwa moja na nchi za Kenya na Uganda huku likitoa pia upatikanaji wa huduma kwa nchi za Rwanda, Burundi na sehemu za mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).
Kwa miongo kadhaa, ziwa hili limekuwa kitovu cha usafiri wa abiria, uvuvi na biashara za kikanda. Hata hivyo, changamoto za miundombinu zilipunguza mchango wake katika mfumo wa kisasa wa usafirishaji. Mageuzi yanayoendelea sasa yanaashiria dhamira ya makusudi kufungua uwezo kamili wa kiuchumi wa ziwa hilo.
Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Plasduce Mbossa anatoa msisitizo mpya wa sera ya kukuza usafiri wa majini kama sehemu ya ajenda ya maendeleo ya muda mrefu ya Tanzania. “Ziwa Victoria ni rasilimali muhimu ya taifa. Uwekezaji wetu una lengo la kuhakikisha kuwa usafiri wa majini unachangia ipasavyo biashara, matumizi ya jamii na ujumuisho wa kanda,” anasema.
Serikali imejitolea karibu Sh bilioni 60 kwa ajili ya upanuzi na uboreshaji wa bandari kuu za Ziwa Victoria zikiwemo Mwanza Kaskazini, Bukoba na Kemondo Bay. Uwekezaji huo unalenga kuongeza uwezo wa kupokea vyombo vikubwa vya majini, kuboresha huduma za abiria, kuongeza ufanisi wa upakuaji na upakiaji mizigo pamoja na kuimarisha usalama wa uendeshaji.
Kwa mujibu wa Mbossa, uboreshaji huo kwa pamoja unalenga kushughulikia idadi kubwa zaidi ya mizigo na abiria na kuruhusu meli kubwa za kisasa kutoa huduma. Kwa mujibu wa taarifa, ikiwa ndiyo kitovu kikuu cha ziwa, Bandari ya Mwanza Kaskazini inaendelezwa ili kuhudumia ongezeko la mizigo na abiria.

Kuhusu Bandari ya Bukoba taarifa zinasema inaboreshwa ili kutoa huduma bora zaidi kwa Mkoa wa Kagera na masoko ya mpakani. Bandari ya Kemondo Bay nayo inatarajiwa kuwa kituo muhimu cha kuhudumia visiwa na kuimarisha shughuli za vivuko vya kisasa.
Umuhimu wa kimkakati wa uwekezaji huu katika bandari unaongezwa na maendeleo ya mradi wa Reli ya Kisasa (SGR) nchini Tanzania. Nafasi ya Mwanza kama kitovu kinachounganisha reli na usafiri wa majini inaruhusu mizigo inayoingia kutoka Bandari ya Dar es Salaam kusafirishwa kwa urahisi kupitia Ziwa Victoria kwenda nchi jirani.
Mbossa anasema: “Uunganishaji kati ya bandari za Ziwa Victoria na SGR umepangwa kimakusudi. Unarahisisha usafirishaji wa mizigo kutoka Bahari ya Hindi hadi maeneo ya ndani na nchi Jirani.” Tayari hatua kubwa zimefikiwa katika utekelezaji wa mradi wa SGR.
Vipande vya Dar es Salaam hadi Morogoro na Morogoro hadi Dodoma vinafanya kazi na hali hiyo kimsingi, imepunguza kwa kiasi kikubwa muda wa safari kati ya Pwani na katikati ya Tanzania. Ujenzi unaendelea katika sehemu za Dodoma hadi Tabora na Tabora hadi Isaka ambavyo ni muhimu kwa kuunganisha reli hiyo na Kanda ya Ziwa.
Baada ya kukamilika kwa kipande cha Isaka hadi Mwanza, Bandari ya Mwanza itaunganishwa moja kwa moja na mtandao wa kitaifa wa reli jambo litakaloongeza nafasi ya Ziwa Victoria kama kitovu cha usafirishaji wa kikanda.
Kwa mujibu wa mkurugenzi kuu huyo wa TPA, muunganiko huo wa reli na usafiri wa majini unatarajiwa kuwezesha usafirishaji wa mizigo ya biashara kwa urahisi kwenda nchi jirani, kupunguza utegemezi wa usafiri wa barabara wa umbali mrefu na kupunguza gharama za usafiri.
Aidha, unaimarisha nafasi ya Tanzania kama lango bora la nchi za Maziwa Makuu katika kufikia masoko ya kimataifa. Uwezo wa uendeshaji katika ziwa hilo unaimarishwa kupitia ujenzi wa meli mpya na uboreshaji wa meli zilizopo.
Mbali na meli mpya ya MV Mwanza Hapa Kazi Tu, meli kama MV Victoria, MV Butiama, MV Umoja na MV Kaawa zinaendelea kutoa huduma za abiria, mizigo na usafiri kwa visiwa. “Lengo letu ni kuimarisha mfumo mzima wa usafiri. Tunazindua meli za kisasa huku zile zilizopo zikiendelea kutoa huduma ili kuhakikisha uendelevu wa safari ndani ya ziwa,” anasema Mbossa.
MV Mwanza Hapa Kazi Tu iliyojengwa kwa gharama ya Sh bilioni 89.7 ni moja ya uwekezaji mkubwa katika usafiri wa majini nchini. Meli hiyo ina uwezo wa kubeba abiria 1,200, magari na mizigo mikubwa, ikiwa na viwango vya juu vya usalama na ufanisi, sambamba na miundombinu mipya ya bandari.
Zaidi ya kuongeza ufanisi wa usafirishaji, uhuishaji wa usafiri katika Ziwa Victoria una manufaa mapana ya kijamii na kiuchumi. Usafiri bora wa maji unasaidia minyororo ya thamani ya kilimo na uvuvi kwa kurahisisha upatikanaji wa masoko.
Aidha, aina hii ya usafiri huchochea utalii na kutoa ajira kupitia shughuli za bandari, huduma za meli na biashara zinazohusiana. Kwa jamii za mwambao na visiwani, uboreshaji huu unarahisisha upatikanaji wa elimu, huduma za afya na masoko ya biashara.
Katika ngazi ya kikanda, usafiri imara wa ziwa unazidi kuimarisha biashara kati ya nchi za Maziwa Makuu na kuunga mkono juhudi za ujumuishaji wa kanda ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC). Katika ufafanuzi wake,
Mbossa anasema: “Lengo letu ni kuwa na mfumo wa usafiri unaounganisha reli, maji na barabara kwa ufanisi. Mtazamo huu wa ujumuishaji unaimarisha ushindani wa taifa na kuchochea maendeleo jumuishi.”
Kadri ujenzi wa reli ya SGR unavyoendelea kuelekea Kanda ya Ziwa na uboreshaji wa bandari unavyokaribia kukamilika, nafasi ya Ziwa Victoria katika mfumo wa usafiri wa Tanzania inazidi kuimarika. Uoanaji wa bandari za kisasa, meli zenye uwezo mkubwa na reli yenye uwezo wa juu unaonesha mwelekeo thabiti wa maendeleo ya miundombinu ya kisasa na kwa njia ya usafiri mchanganyiko.
Kupitia uwekezaji endelevu na mipango iliyoratibiwa, Tanzania inainua upya Ziwa Victoria si tu kama njia ya usafiri, bali kama korido ya kibiashara yenye umuhimu wa kimkakati. Mageuzi hayo yanaonesha dhamira ya taifa kutumia njia za maji za ndani kama injini za biashara, muunganiko wa kikanda na maendeleo ya muda mrefu katika eneo la Maziwa Makuu.
0 Comments