
KAMPUNI ya Ujenzi na Ukarabati wa Miundombinu ya Usafi rishaji na Usambazaji wa Umeme (ETDCO) imesaini mikataba ya Sh bilioni 95.2 kutekeleza miradi ya Wakala wa Umeme Vijijini (REA) ya kusambaza umeme katika vitongoji 620 vya mikoa ya Katavi na Ruvuma.
Akizungumza wakati wa hafla ya utiaji saini uliofanywa mjini Dodoma, Kaimu Meneja Mkuu wa ETDCO, Richard Mwanja ameishukuru Wizara ya Nishati pamoja na REA kwa imani waliyoipa kampuni hiyo na kusema wamejipanga vizuri kutekeleza mradi huo kwa wakati.
Amesema miradi hiyo inatarajiwa kukamilika ndani ya kipindi cha miaka mitatu ambapo itanufaisha zaidi ya wananchi 19,950 katika mikoa ya Katavi na Ruvuma. “Miradi hii ni kicheko kwa wananchi wa maeneo husika, tunatarajia kutoa ajira kwa zaidi ya wananchi 500 zikiwemo za moja kwa moja, hivyo tunawahimiza wananchi kuchangamkia fursa hii pindi utekelezaji ukianza,” alisema.
Amefafanua miradi hiyo, Mwanja alisema mkoani Katavi, Sh bilioni 37.9 zitatumika kusambaza umeme katika vitongoji 262 na kuwanufaisha wananchi 8,414 huku mkoani Ruvuma Sh bilioni 57.3 zitatumika kusambaza umeme katika vitongoji 358 na wananchi 11,536 watanufaika. SOMA: REA yazindua kituo cha kusambaza umeme Mtera
Mwanja amesema kukamilika kwa miradi hiyo kutafungua fursa za kijamii na kiuchumi, kuimarisha shughuli za maendeleo na kuchangia ustawi endelevu wa taifa. Hadi sasa ETDCO imekamilisha ujenzi wa miradi yenye urefu wa zaidi ya kilometa 5,061 ya usafirishaji na usambazaji wa umeme nchini, ikiwa ni pamoja na kuunganisha Mkoa wa Katavi na gridi ya taifa.
Hatua hiyo ni mapinduzi ya maendeleo hususani katika maeneo ambayo nishati ya umeme ilikuwa haijafika. “Tumekamilisha miradi mikubwa na midogo mbalimbali ya kusafirisha umeme na kusambaza nishati hiyo kwa wananchi, tumeshafanya kazi hiyo kwa urefu wa kilometa 5,061 katika maeneo tofauti nchini,” alisema
Mhandisi Mkuu wa ETDCO, Mustapha Himba. Alisema katika miradi ya kusafirisha umeme kilometa 578 zimejengwa ambayo ni pamoja na ule wa msongo wa kilovolti 132 kutoka Mtwara hadi Mahumbika yenye kilometa 80, mradi kutoka Tabora-Urambo kilometa 115 na Tabora-Katavi kilometa 383.
Pia, miradi ya kusambaza umeme uliyokamilika ina urefu wa kilometa 4,483 na imehusisha miradi mbalimbali ikiwemo ile ya REA, Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) na ya kampuni za madini ikiwemo ya STAMIGOLD na GGM. Amesema katika hilo wameunganisha vijiji 291 na umeme wa REA katika mikoa ya Katavi, Arusha, Mbeya, Kigoma,Mwanza na Geita.
Aidha, vitongoji 105 mkoani Mbeya vinaendelea kuunganishwa na umeme, hatua ambayo inafungua fursa kwa wananchi kujiongezea kipato kwa kutumia nishati hiyo kutekeleza miradi ya kiuchumi. Himba amesema ETDCO pia imewaunganisha wateja 18,000 wa njia moja umeme na wateja 3,000 wa njia kubwa nishati hiyo.
Kusainiwa kwa miradi hiyo ni kicheko kwa wananchi wa maeneo husika kwani kampuni hiyo inatarajia kutoa ajira zikiwemo za moja kwa moja kwa zaidi ya wananchi 500 wa maeneo mradi unakopita.
0 Comments