MOROCCO; Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Paul  Makonda amekutana na Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) Dk Patrice Motsepe jijini Rabat, Morocco na kukabidhi barua kutoka kwa Rais wa Tanzania, Dk Samia Suluhu Hassan.

Pamoja na kukabidhi barua hiyo Makonda aliyeongozana na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo na Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa amemhakikishia Dk Motsepe kuwa Rais Samia yupo tayari wakati wote kushirikiana na CAF katika utekelezaji wa mipango mbalimbali ya maendeleo ya kandanda, ikiwemo mashindano mbalimbali.

Amesema Tanzania imepiga hatua kubwa katika maandalizi ya kuwa wenyeji wa AFCON 2027 sambamba na Kenya na Uganda na kwamba imedhamiria kuonesha tofauti kubwa na mashindano yaliyopita.

Aidha Makonda amemuomba Dk Motsepe kuiangalia Tanzania kimkakati, ili mipango inayowekwa na Serikali ipate mafanikio makubwa yanayotarajiwa.

Kwa upande wake Dk Motsepe amemshukuru Rais Samia kwa kumuandikia barua na salamu zake za upendo na ushirikiano kwa CAF na amemhakikishia kuwa CAF ipo tayari kufanya kazi bega kwa bega na Tanzania,  ili kufikia maendeleo makubwa katika kandanda.

Motsepe ameelezea kufurahishwa na jitihada kubwa zilizofanywa na Rais Samia na Serikali anayoiongoza katika maendeleo ya mpira, ikiwemo ujenzi wa miundombinu, kufanya mashindano ya CHAN 2024 kwa mafanikio makubwa na maandalizi mazuri yanayoendelea kuelekea AFCON 2027.

Amesema CAF itatuma timu ya wataalamu kwenda Tanzania kushirikiana na Serikali na wadau mbalimbali katika kukamilisha maandalizi makubwa ya AFCON 2027, ambayo yanatarajiwa kushirikisha nchi 28 badala ya 24.

Pia Motsepe ameahidi  kutembelea Tanzania hivi karibuni kujionea maandalizi mbalimbali ya AFCON 2027 na kukutana na viongozi kwa mazungumzo.