Kiongozi wa Israel, Benjamin Netanyahu, ameitisha mkutano na washauri wake wakuu kujadili kile Rais wa Marekani Donald Trump anachokiita “Bodi ya Amani” kwa Gaza, baada ya Israel kusema haikushirikishwa katika mazungumzo kuhusu muundo wa moja ya vyombo vya chini vya bodi hiyo.
Marekani ilitangaza Jumamosi majina ya wajumbe wa kwanza wa Bodi ya Utendaji ya Gaza, wakiwemo Waziri wa Mambo ya Nje wa Uturuki, afisa mmoja wa Qatar, aliyekuwa Waziri Mkuu wa Uingereza Tony Blair, pamoja na mkwe wa Trump, Jared Kushner.
Ofisi ya Netanyahu baadaye ilisema uteuzi huo “haukuratibiwa na Israel na unakwenda kinyume na sera yake.”
Bodi ya Amani ni sehemu ya mpango wa vipengele 20 wa Trump unaolenga kumaliza vita kati ya Israel na Hamas, na inatarajiwa kusimamia kwa muda uendeshaji wa Ukanda wa Gaza.
Muundo kamili wa bodi hiyo, ambayo pia itasimamia ujenzi upya wa Gaza, bado haujawekwa wazi, na wajumbe wengine bado wanaendelea kualikwa.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Ikulu ya Marekani (White House), “Bodi ya Utendaji ya Gaza” itakuwa na jukumu la kusimamia shughuli zote za utekelezaji wa kazi zinazofanyika nchini humo kwa niaba ya chombo kingine cha kiutawala kinachoitwa Kamati ya Kitaifa ya Usimamizi wa Gaza (NCAG).
Chombo cha pili, kinachoitwa “Bodi ya Utendaji ya Waanzilishi”, ambacho pia kinawajumuisha Jared Kushner na Tony Blair, kitakuwa na jukumu la ngazi ya juu katika masuala ya uwekezaji na diplomasia.

0 Comments