Marekani imeonyesha upinzani wake dhidi ya uamuzi wa Afrika Kusini kushiriki katika zoezi la kijeshi la majini la kimataifa linalohusisha Iran, ikiielezea Tehran kama “mhusika anayevuruga utulivu wa kimataifa na mfadhili wa ugaidi.”
Marekani imeonya kuwa ushiriki wa Iran katika zoezi hilo unatishia usalama wa kikanda na wa baharini.
Kupitia taarifa rasmi, Ubalozi wa Marekani nchini Afrika Kusini ulisema Washington ilipokea kwa “wasiwasi mkubwa na hofu” taarifa kuwa Waziri wa Ulinzi wa Afrika Kusini pamoja na Jeshi la Ulinzi la Taifa la Afrika Kusini (SANDF) waliendelea kuruhusu ushiriki wa Iran katika mazoezi hayo yanayoendelea, licha ya madai kuwa kulikuwa na maelekezo ya serikali yaliyopinga hatua hiyo.
Ubalozi huo ulisisitiza kuwa kuijumuisha Iran katika mazoezi ya pamoja ya kijeshi, kwa namna yoyote ile, kunadhoofisha usalama wa baharini na uthabiti wa kikanda.
Taarifa hiyo ilieleza kuwa ni jambo “lisilokubalika kimaadili” kwa Afrika Kusini kuwapokea wanajeshi wa Iran wakati ambapo, kwa mujibu wa Marekani, mamlaka za Iran zinaendelea kuwanyanyasa raia wake kwa kuwapiga risasi, kuwafunga gerezani na kuwatesa wale wanaoshiriki shughuli za kisiasa kwa amani.
Aidha, ubalozi huo uliikosoa sera ya kigeni ya Afrika Kusini, ukidai kuwa nchi hiyo haiwezi kudai kusimamia misingi ya haki na usawa kimataifa huku ikiimarisha uhusiano na Iran.
Ubalozi uliongeza kuwa kuruhusu vikosi vya kijeshi vya Iran kufanya shughuli katika maji ya Afrika Kusini, au kuonyesha mshikamano wa kisiasa na Tehran, kunavuka mipaka ya sera ya kutofungamana na upande wowote.
“Hatua hii ni sawa na kuchagua kusimama upande wa utawala unaowakandamiza raia wake kwa ukatili na kujihusisha na vitendo vya kigaidi,” taarifa hiyo ilisema.
Malalamiko haya ya kidiplomasia yanajiri wakati Afrika Kusini ikiandaa Zoezi la WILL FOR PEACE 2026, zoezi la kimataifa la majini linalohusisha majeshi ya wanamaji kutoka China, Urusi, Iran na Afrika Kusini, huku China ikiwa kiongozi wa zoezi hilo.
Zoezi hilo lilianza rasmi tarehe 10 Januari 2026 kwa gwaride la ufunguzi lililofanyika katika mji wa Simon’s Town, likiashiria mwanzo wa shughuli za pamoja zinazofanyika katika maeneo ya mafunzo na katika maji ya eneo la Afrika Kusini.
Kwa mujibu wa Jeshi la Afrika Kusini, zoezi hilo linalenga kuziunganisha nchi wanachama wa 'BRICS Plus' katika kuimarisha usalama wa baharini, kuongeza uwezo wa kufanya kazi kwa pamoja, na kuendeleza ushirikiano wa kijeshi wa kimataifa.
Brics iliundwa kutafuta njia za kuleta mageuzi katika taasisi za fedha za kimataifa kama vile IMF na Benki ya Dunia, ili kuunda "sauti kubwa na uwakilishi" kwa mataifa yanayoibukia kiuchumi.
Hadi sasa, Afrika Kusini haijatoa majibu ya kina hadharani kuhusu ukosoaji wa Marekani, ingawa maafisa wake wamewahi kusisitiza kuwa mazoezi ya aina hiyo yanaendana na sera ya nchi ya kutofungamana na upande wowote pamoja na dhamira yake ya kuendeleza ushirikiano wa kimataifa.

0 Comments