Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, amempongeza Rais wa Jamhuri ya Uganda, Yoweri Kaguta Museveni, kwa kuchaguliwa tena katika Uchaguzi Mkuu uliokamilika wiki jana.
Katika ujumbe wake wa pongezi, Rais Samia amesema ushindi wa Rais Museveni unaakisi imani, heshima na matarajio makubwa ambayo wananchi wa Uganda wanayo kwa uongozi wake na maono yake ya kuiletea nchi yao maendeleo endelevu.
“Kwa niaba ya Serikali na wananchi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, napenda kutoa pongezi za dhati kwako Mheshimiwa Rais mteule Yoweri Museveni kwa kuchaguliwa tena. Ushindi wako unaonesha imani na dhamana waliyo nayo wananchi wa Uganda katika uongozi wako,” amesema Rais Samia.
Aidha, Rais Samia ameonesha nia ya kuendelea kufanya kazi kwa karibu na Rais Museveni katika kuimarisha na kukuza zaidi uhusiano wa kindugu na wa kihistoria uliopo kati ya Tanzania na Uganda, kwa manufaa ya wananchi wa nchi zote mbili.
Rais Samia amesisitiza kuwa Tanzania itaendelea kushirikiana na Uganda katika nyanja mbalimbali zikiwemo maendeleo ya kiuchumi, biashara, usalama na ustawi wa kijamii, kwa lengo la kuimarisha mshikamano wa kikanda na maendeleo ya Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Halkadhalika, Rais Samia alimtakia Rais Museveni kila la heri na mafanikio katika muhula wake mpya wa uongozi.

0 Comments