Rais mteule wa Uganda, Yoweri Museveni, ametoa shukrani kwa ushindi wake katika uchaguzi mkuu, huku akibainisha kwamba alitarajia kupata idadi kubwa zaidi ya kura.

Jumamosi, Tume ya Uchaguzi ya Uganda ilimtangaza Museveni mshindi rasmi wa uchaguzi huo baada ya kupata asilimia 71 ya kura zilizopigwa.

Mpinzani wake mkuu, Bobi Wine, alipata asilimia 24 tu.

"Sasa, ninataka kushukuru Mungu kwa ushindi huu, na ushindi mwingine wote ambao tumekuwa nao katika miaka hamsini iliyopita - miaka hamsini na mitano ya mapambano tangu 1971 ...." Museveni alisema

Rais mteule aliongeza:

"Milioni kumi ya watu wangu hawakujitokeza kupiga kura. Wangeaibishwa sana (upinzani)…… kama wanachama wetu wote wangetokea, hakungekuwa na upinzani wowote nchini Uganda, ninakuhakikishia" alisema.

Idadi ya wapiga kura waliosajiliwa katika uchaguzi huu ilikuwa milioni 22, lakini asilimia 52 tu ndio waliopiga kura, kiwango cha chini kabisa katika historia ya uchaguzi nchini Uganda.

Kiwango cha juu zaidi kiliripotiwa katika uchaguzi wa mwaka 1980, kilichokadiria kuwa takribani asilimia 85.

Museveni alitoa hotuba Jumapili nyumbani kwake Rwakitura, magharibi mwa Uganda, wakati wa sherehe ya kupokea taarifa ya ushindi, iliyohudhuriwa na wanachama wa chama chake na viongozi wa dini miongoni mwa wengine.

Bila kutoa ushahidi wowote, Museveni alidai kuwa mpinzani wake, Bobi Wine, alikuwa akishirikiana na maslahi ya kigeni na kujaribu kutoa hongo ya shilingi 10,000 kwa kila raia wa Uganda, kwa nia ya kudhoofisha utulivu wa taifa kwa njia inayofanana na Libya.

Viongozi kadhaa wa kigeni, wakiwemo Mwenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika na marais wa Rwanda, Kenya, na Somalia, wamemtumia ujumbe wa pongezi kwa Rais Museveni kupitia mitandao yao ya kijamii.

Kuhusu mipango ya muhula wake mpya, Museveni alisema kwamba uundaji wa ajira utazingatia kilimo, viwanda, na sekta binafsi, badala ya ajira za umma.

Aliongeza kuwa mapato yatakayopatikana kutokana na uzalishaji wa mafuta unaotarajiwa kuanza mwishoni mwa mwaka huu yatawekezwa katika miradi ya taifa yenye manufaa ya muda mrefu.

“Mafuta yetu yataanza kuuzwa mwaka huu. Pesa hizi lazima zitumike katika miradi ya kudumu, kama vile reli, vituo vya nguvu, barabara, na elimu ya sayansi,” alisema.

Chama kikuu cha upinzani, National Unity Platform (NUP), bado hakijatoa tathmini rasmi ya matokeo, lakini kimekataa matokeo hayo kwa ujumla.

Kiongozi wake, Bobi Wine, ameielezea matokeo kuwa ni ya uwongo.

Bobi Wine bado yupo katika kizuizi cha siri na amewaambia waandishi wa habari kuwa ana hofu ya maisha yake, akidai kuwa jeshi limevamia nyumba yake kwa nia ya kumdhuru.

Ameutaka umma kupinga matokeo hayo kwa njia ya amani. Hadi sasa, hakuripotiwa kuibuka kwa maandamano makubwa au ya upinzani kwa wingi nchini Uganda.