RAIS wa Shirikisho la Kandanda Duniani (FIFA) Gianni Infantino amesema shirikisho hilo lipo tayari kushirikiana na Tanzania katika programu zake za maendeleo ambazo zitasaidia kutengeneza fursa kwa vijana kunufaika na mchezo wa mpira wa miguu ikiwemo ujenzi wa miundombinu na uendelezaji wa vituo vya ufundi.

Infantino amesema hayo alipokutana na kufanya mazungumzo na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Paul Makonda na ujumbe wake kando ya fainali ya Kombe la Mataifa ya Afrrika (AFCON 2025) iliyofanyika jijini Rabat, Morocco.

Infantino ameipongeza Tanzania kwa kazi kubwa iliyofanywa na inayoendelea kufanywa na Serikali ya ujenzi wa miundombinu ya michezo kuelekea AFCON 2027 na amesema FIFA itaunga mkono jitihada hizo.

SOMA: Makonda awasili Morocco

Kwa upande wake Waziri Makonda amemshukuru Infantino kwa ushirikiano mkubwa anaoutoa kwa Tanzania katika maendeleo ya mchezo wa mpira wa miguu na amemhakikishia kuwa Rais Samia Suluhu Hassan na Serikali anayoiongoza inaunga mkono jitihada hizo na ipo tayari kushirikiana na FIFA.

Makonda amemkaribisha Tanzania Infantino na amemwambia Tanzania ipo tayari kuwa mwenyeji wa matukio mbalimbali ya FIFA ikiwemo mashindano mbalimbali, mikutano na ziara za viongozi na wataalamu.

Halikadhalika Makonda amemualika Infantino kuja Tanzania kuangalia maandalizi ya kuelekea uenyeji wa AFCON.