Katibu wa Baraza Kuu la Usalama wa Kitaifa la Iran, Ali Larijan amesema Tehran itaruhusu ziara katika vituo vya chini ya ardhi na chini ya milimani ili kuthibitisha kwamba mpango wake wa nyuklia ni kwa ajili ya amani.
Katika mahojiano na Al Jazeera, Larijani amesema "ili kushughulikia wasiwasi wa wengine, ni lazima tukubali kanuni za Shirika la Kimataifa la Nishati ya Nyuklia (IAEA). Tulipokubali mkataba wa NPT, pia tulikubali mfumo wa ufuatiliaji wa Shirika hilo. Ukaguzi unaweza kubadilishwa; kila mwezi au hata kila siku, ili kubaini shughuli yoyote ya kutiliwa shaka."
Katibu wa Baraza la Usalama la Kitaifa la Iran amesema: "Hata kama teknolojia hiyo iko chini ya ardhi au mlimani, hakuna tatizo; Shirika linaweza kuifuatilia na tunaruhusu ufuatiliaji huu."
Alisisitiza kwamba "suala la makombora halina uhusiano wowote na mazungumzo na halitajadiliwa katika mazungumzo haya."
Kwa upande mwingine rais wa Marekani, Donald Trump amesema masafa ya makombora ya Iran ni mojawapo ya masharti yake ya kufanya mazungumzo na Iran.
Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu pia ameonya jana kwamba katika makubaliano yoyote na Iran, kuacha kurutubisha urani hakutatosha na miundombinu yote ya nyuklia lazima ivunjwe.
Pia alisisitiza kwamba makubaliano yoyote na Iran lazima yajumuishe suala la makombora ya balestiki.

0 Comments