
RAIS Samia Suluhu Hassan ameendeleza nafasi ya Tanzania katika jukwaa la Afrika na kimataifa kama sehemu ya kuimarisha diplomasia ya kiuchumi ili kufi kia malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
Taarifa ya Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu, Bakari Machumu imeeleza Rais Samia ameendelea kuimarisha diplomasia ya kimkakati kupitia mazungumzo ya pande mbili aliyoyafanya na viongozi wa nchi mbalimbali kando ya Mkutano wa 39 wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Umoja wa Afrika (AU) jijini Addis Ababa, Ethiopia.
Jana alizungumza na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Comoro, Azali Assoumani kujadili kuimarisha ushirikiano wa kikanda hususani katika sekta za biashara, utalii, usafirishaji wa baharini na masuala ya usalama. Rais Assoumani amemshukuru Rais Samia kwa ushirikiano wa pamoja na mchango wa Tanzania nchini kwake hususani katika kuimarisha huduma za afya, biashara na masuala ya usalama.
Ameshukuru mchango wa Tanzania katika huduma za kibingwa za matibabu kwa wananchi wa Comoro. Kupitia mazungumzo hayo, Rais Assoumani pia alionesha nia ya kufanya ziara ya kiserikali nchini Tanzania ambapo, Rais Samia aliridhia ombi hilo. Juzi Rais Samia alikutana na kuzungumza na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Shirikisho la Ethiopia, Dk Abiy Ahmed Ali kabla ya ufunguzi rasmi wa Mkutano Mkuu wa AU.
Viongozi hao wamejadili kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia, kukuza biashara na uwekezaji na ushirikiano katika sekta za usafiri wa anga na usimamizi wa rasilimali za maji. Viongozi hao pia walibadilishana uzoefu kuhusu mwelekeo wa uchumi wa nchi zao. SOMA: Rais Samia kuanza ziara China
Ethiopia inalenga kukuza uchumi kwa asilimia 10.2 na Tanzania inatarajia kufikia ukuaji wa asilimia 6.5 kama sehemu ya jitihada za kuimarisha ustawi wa wananchi wa nchi zote mbili. Februari 13, Rais Samia amezungumza na Rais wa Jamhuri ya Angola, João Lourenço kuhusu kukuza ushirikiano wa kiuchumi, biashara, uwekezaji na maendeleo ya viwanda kati ya Tanzania na Angola.
Rais Lourenço wa Angola amekubali kufanya ziara ya kiserikali nchini Tanzania na akakubali kuwa mgeni rasmi katika Maonesho ya Kimataifa ya Biashara ya Sabasaba mwaka 2026. Viongozi hao wamesisitiza umuhimu wa kuimarisha uhusiano wa kihistoria na ushirikiano wa kimkakati kwa manufaa ya maendeleo ya kiuchumi na ustawi wa wananchi wa pande zote mbili hususani katika sekta za nishati, madini, viwanda na miundombinu.
0 Comments