Polisi wa Indonesia wamesema Jumatano kwamba rubani na rubani msaidizi wa ndege ndogo ya kibiashara wamefariki baada ya washambuliaji wasiojulikana kuifyatulia risasi ndege yao ilipokuwa ikitua katika eneo la mashariki mwa nchi ya Papua.

Ndege ya Smart Air, iliyokuwa na abiria 13 pamoja na marubani, ilitua katika uwanja wa ndege wa Korowai huko Boven Digoel, eneo la Papua Kusini, Jumatano saa 11.17 asubuhi kwa saa za eneo, msemaji wa polisi wa eneo hilo Cahyo Sukarnito aliambia Reuters.

Wakati ufyatuaji risasi ulipoanza, marubani na abiria waliiacha ndege hiyo na kuelekea eneo la msitu karibu na uwanja wa ndege, Ndege ya Smart Air ilisema.

Rubani na rubani msaidizi waliuawa lakini abiria wote walikuwa salama.

Cahyo alisema haijafahamika ni nani aliyetekeleza shambulio hilo, baada ya kuulizwa kuhusu uwezekano wa kuhusika kwa makundi ya waasi ya Papua.