Rais Donald Trump atakuwa mwenyeji wa Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu katika Ikulu ya White House siku ya Jumatano, huku mvutano ukiendelea kuongezeka katika eneo la Mashariki ya Kati na mazungumzo yakizidi kupamba moto kuhusu kuzuia mpango wa silaha za nyuklia wa Iran.
Netanyahu anatarajiwa kumshinikiza Trump kutekeleza makubaliano ambayo yatasimamisha urutubishaji wa uranium ya Iran, na kudhibiti uungaji mkono wake kwa vikundi vya wakala kama Hamas na Hezbollah.
"Nitawasilisha kwa rais mtazamo wetu kuhusu kanuni za mazungumzo haya," Netanyahu aliwaambia waandishi wa habari kabla ya kuondoka kuelekea Marekani.
Iran imesema haitazuia urutubishaji wa madini ya uranium isipokuwa mataifa ya Magharibi yatapunguza vikwazo ambavyo vimezorotesha uchumi wake.
Ziara ya Netanyahu siku ya Jumatano inaashiria safari yake ya sita nchini Marekani tangu Trump arejee madarakani - zaidi ya kiongozi yeyote duniani.
Mshirika wa karibu wa Trump, Netanyahu kwa muda mrefu amekuwa akisema kuwa Iran inawakilisha tishio la usalama lililopo kwa Israeli na ameisukuma Marekani kuzuia ushawishi wa Tehran katika eneo hilo.
"Waziri Mkuu anaamini kwamba mazungumzo yoyote lazima yajumuishe kupunguza makombora ya balestiki na kukomesha msaada kwa mhimili wa Iran," ofisi ya Netanyahu ilisema katika taarifa kabla ya safari yake.
Ziara hiyo inakuja huku Marekani ikiongeza uwepo wake wa kijeshi katika Mashariki ya Kati, huku Trump akiionya Tehran kuchukua hatua iwapo itashindwa kufikia makubaliano ya nyuklia.

0 Comments