
WAZIRI Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba ameiagiza Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) isimamie shule zote nchini ziwe na matundu ya vyoo ya kutosha.
Dk Mwigulu ametoa agizo hilo wakati wa halfa ya uwekaji jiwe la msingi kwenye tawi la Chuo Kikuu Mzumbe wilayani Mkinga mkoani Tanga . Wakati wa tukio hilo alipokea taarifa kuhusu ujenzi wa matundu ya vyoo katika Shule ya Sekondari Kigongoi, Kituo cha Afya cha Malamba na ujenzi wa matundu ya vyoo katika Shule ya Msingi Perani katika Wilaya hiyo ya Mkinga mkoani Tanga.
Mwigulu amemuagiza Waziri wa Tamisemi, Profesa Riziki Shemdoe awaandikie barua wakurugenzi na maofisa tarafa nchi nzima ili wasimamie utekelezaji wa agizo hilo kwenye maeneo wanayoongoza. “Waziri wa Tamisemi waandikie barua maofisa tarafa wa mikoa na wakurugenzi wa nchi nzima, tutakapomaliza miezi sita ya bajeti mpya sitaki kusikia shule imekosa matundu ya vyoo,” alisema.
Dk Mwigulu amesema utekelezaji wa agizo hili ufanyike wakati mchakato wa kuandaa bajeti mpya ya mwaka wa fedha 2026/2027. “Haya si mambo ya kujadiliana hivi hadharani, tunaweza kuwa na shule halafu haina matundu ya vyoo, unawezaje kuwa na mrundikano wa watoto 300 halafu hamna vyoo na sisi tupo maofisini, tuna magari, gari moja tu inajenga matundu ya vyoo vya halmashauri yote, mnaombaje fedha za magari mnakosa matundu ya vyoo,” alisema.
Dk Mwigulu amesema anashangaa kuona katika karne hii katika nchi ambayo ina hadhi ya kipato cha kati kuna halmashauri yenye shule ambayo inakosa matundu ya vyoo. “Haya ni mambo yanayoturejesha kwenye ujima na mambo yanayotia aibu, hatuwezi kuwa na miradi mikubwa kama hii halafu tuwe na eneo ambalo halina matundu ya vyoo, huu ni uzembe unaotokana na watu wetu wasiotembelea maeneo yao ya kazi,” alisema Dk Mwigulu.
Ameongeza : “Ziara zitakazofuata baada ya miezi sita ya bajeti nikikuta kuna halmashauri ina shule ya msingi, ina shule ya sekondari haina matundu ya vyoo au ina mapungufu ya matundu ya vyoo, Mkurugenzi utakuwa umepoteza kazi yako utatufaa nini ikiwa hata matundu ya vyoo huwezi kusimamia yakajengwa?”
Dk Mwigulu aliziagiza wizara zote zinazosimamia ujenzi wa miundombinu ikiwemo barabara, maji na umeme zisimamie ukamilishaji wa miundombinu kwenye chuo hicho kwa sababu kimepanga kuanza kutoa huduma mwaka mpya wa masomo unaotarajia kuanza Oktoba mwaka huu.
“Niwaelekeze watu wa nishati meneja wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) pamoja na makao makuu mjipange ili tusije kukamilisha upande mwingine wa miundombinu tukakwama kwenye upande mwingine wa umeme,” alisema.
Ameongeza : “Jipangeni hizi kazi zote ziende sambamba ziishe kwa wakati, kama mlivyomsikia makamu mkuu wa chuo alisema mwaka wa kitaaluma ukianza wanatarajia kuanza, sisi tusiwe kikwazo cha mpango wao huo wa kuanza udahili mwaka wa taaluma utakapoanza”.
Mradi huo wa ujenzi wa Chuo kikuu cha Mzumbe tawi la Mkinga unatekelezwa kwa zaidi ya Sh bilioni 12. Ujenzi huo unahusisha miundombinu ya kujifunzia na kufundishia pamoja na majengo mengine ikiwemo jengo la taaluma, hosteli mbili za wanafunzi ambayo kila moja ina uwezo wa kubeba wanafunzi 180. SOMA: Dk Mwigulu kuzindua miradi ya utalii kesho
0 Comments