WAZIRI Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba amezindua na kukabidhi miundombinu 21 ya utalii yenye thamani ya Sh billioni 114.62.

Amesema ujenzi wa miradi hiyo ambayo imejengwa kupitia mradi wa kimkakati wa kukuza na kuendeleza utalii Ukanda wa Kusini ni sehemu ya maono ya Rais Samia Suluhu Hassan yanayolenga katika kukuza sekta ya utalii nchini.

“Hii ndio imekuwa sifa ya Mheshimiwa Rais Dkt. Samia, maneno kidogo, matendo zaidi, amesema”

Amesema hayo leo Fenruari 11, 2026 wakati alipozindua uwanja wa ndege Mtemere uliopo katika kijiji cha Mloka, mkoani Pwani kwenye hifadhi ya Taifa ya Nyerere. Uwanja huo ni sehemu ya miradi 21 iliyozinduliwa.

Ameitaja miradi hiyo kuwa ni Malango ya kuingilia hifadhini, vituo vya taarifa kwa wageni, kambi za wageni, eneo la kupumzikia wageni, nyumba za wageni, hosteli za wanafunzi, kituo cha kufuatilia ikolojia, na vituo vya askari.

Kadhalika, Dk Mwigulu ameziagiza mamlaka zote zihakikishe zinaitunza na kuilinda Miundombinu hiyo ambayo imegramu fedha nyingi.

“Hakikisheni miradi hii inatunzwa na kukarabatiwa mara kwa mara ili kuwezesha nchi kufikia malengo ikiwemo kuongeza pato la utalii na kutoa ajira, Wananchi hakikisheni pia mnailinda miundombinu hii,” amesisitiza.

Aidha, Dk Mwigulu ameiagiza Wizara ya Maliasili na Utalii kushirikiana na mashirika ya ndege ikiwemo ATCL ili kuona namna bora ya kutumia fursa ya ujenzi wa uwanja na kuandaa ratiba za ndege Kutoka Dar/Zanzibar – Nyerere – Mikumi-Ruaha-Songwe.

Pia, Dk Mwigulu amesema kuwa Serikali imeendelea kuwekeza katika miundombinu mbalimbali ikiwemo ununuzi wa magari 61 kwa ajili ya shughuli za utalii na doria.

“Vilevile, Serikali imenunua jumla ya mitambo mikubwa 18, malori 46, matrekta 7 na vifaa vingine mbalimbali kwa ajili ya kuendeleza sekta hii ya uhifadhi na utalii,”

“Tutaendelea pia kuweka mazingira wezeshi na rafiki katika kuendeleza sekta ya utalii na uhifadhi kwa kuweka sera ambazo zitawezesha sekta binafsi kuwekeza zaidi katika uhifadhi na utalii kwa maslahi mapana ya Taifa,” amesema.

Awali, Waziri wa Maliasili na Utalii Dk Ashatu Kijaji amesema kuwa katika kipindi cha uongozi wa Rais Samia idadi ya watalii imeongezeka kwa zaidi ya asilimia 149 ikiwa ni ongezeko la watalii 2,294,495 mwaka 2025 kutoka watalii 922, 692.

“ongezeko hili limetokana na uwekezaji mkubwa na wakimkakati katika sekta ya uhifadhi na utalii,” amesema.