

Aidha, Ndejembi aligusia suala la kufikisha umeme kwenye maeneo ya wananchi akieleza kuwa Serikali imejipanga kuhakikisha umeme unatoka kwenye vyanzo vya uzalishaji na kufikia maeneo ya wananchi na ya uzalishaji kama vile migodi viwanda.
Katika jitihada hizo za kufikisha umeme kwa wananchi alisema mradi wa kufikisha umeme wa gridi mikoa ya Mtwara na Lindi kupitia ujenzi wa njia ya umeme ya kV 220 ya Songea- Tunduru- Masasi-Mahumbika unaendelea huku mkandarasi akiwa ameshalipwa shilingi bilioni 83 kwa ajili ya kuendelea na kazi.

Katika hatua nyingine, Waziri wa Nishati aliiagiza TANESCO na Wakala wa Nishati Vijijini ( REA) kuwasiliana na Wabunge wote ambao wana maeneo ambayo ni Manispaa/Majiji/ Halmashauri za Mji lakini yana sura ya vijiji ambayo wananchi wake wanalipa zaidi ya shilingi 27,000 kuunganisha umeme ili kuvitambua vijiji hivyo na kuja na mradi utakaohakikisha wananchi katika vijiji hivyo wanaunganishiwa umeme kwa shilingi 27,000 tu ndani ya mwaka mmoja.
” Serikali hii ya Dk. Samia Suluhu Hassan ni sikivu na haiwezi kuweka matabaka ya wananchi, mtu amekaa ng’ambo moja analipa 27,000 na ng’ambo nyingine analipa 320,000 hili halikubaliki, Serikali imesikia changamoto hii na inaifanyia kazi, tutahakikisha umeme unawaka katika vijiji ambavyo vipo ndani ya miji.” Alisema Ndejembi
Kuhusu suala la kufikisha umeme kwenye Taasisi kama vile shule na zahanati aliitaka REA kufanya tathmini ili kutambua taasisi ambazo hazijapelekewa umeme katika vijiji vyenye umeme ili ziweze kuunganishiwa.

Aidha, kuhusu suala la mafuta alisema kufungwa kwa mlango bahari wa Hormuz kunaleta changamoto kubwa ya upatikanaji mafuta duniani kwani asilimia 20 ya nishati ya mafuta inatoka katika mlango bahari huo lakini kutokana na Serikali ya Tanzania kujali wananchi wake, nchi ina mafuta ya kutosha na hakuna kituo ambacho kimefungwa kwa kukosa nishati hiyo tofauti na baadhi ya maeneo mengine duniani.
Vilevile kuhusu bei ya mafuta alieleza kuwa Serikali inafanya kila jitihada ili ziwe himilivu huku ikihakikisha mafuta yanapatikana muda wote na hifadhi mpya ya mafuta inayojengwa jijini Dar es Salaam eneo la Kigamboni ikitoa hakikisho la uhifadhi wa mafuta.
0 Comments