Msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Iran anasema jibu kwa wapatanishi wanaofanya kazi ya kukomesha vita kati ya Marekani na Israeli na Iran limeandaliwa.
Inafuatia ripoti kutoka Reuters, zikinukuu vyanzo visivyotajwa majina, kwamba Pakistan ina jukumu kubwa katika kuandaa mpango mpya wa kukomesha mgogoro huo.
Esmail Baghaei ananukuliwa na shirika la habari la serikali IRNA akisema kwamba mpango huo wa vipengele 15 uliotolewa kupitia wapatanishi na Marekani "haukukubalika kwetu kwa vyovyote vile".
Anaongeza kuwa mazungumzo ya kukomesha mgogoro huo "hayaendani na masharti ya mwisho na vitisho vya kufanya uhalifu wa kivita," kufuatia onyo la Trump kwamba Marekani italenga miundombinu ya raia ya Iran ikiwa Mlango-Bahari wa Hormuz hautafunguliwa tena.
Badala yake, anasema Iran imekusanya madai "kulingana na maslahi na mawazo yetu wenyewe". "Tangu mwanzo tulijua tunachotaka na ni mistari gani myekundu ambayo hatukuwa tayari kuvuka, na msimamo wetu uko wazi hata sasa. Tangu wakati mjadala huu ulipoanza, majibu yetu yalikuwa tayari," anasema, akiongeza kuwa Iran imeunda majibu yake na "itatoa maelezo kwa wakati unaofaa".

0 Comments