![]()
VIONGOZI wa dini yaKikristo wamewataka waumini wa dini hiyo na Watanzania kuenzi umoja na kuendelea kushikamana katika upendo na kutumia Sikukuu ya Pasaka kufufua yaliyo mema huku wakipinga matendo maovu.
Pia wameitaka jamii kuzingatia suala la malezi mema kwa watoto na kutoa mwongozo unaofaa miongoni mwa vijana ili jamii iwe na kizazi chenye maadili siku zijazo. Wito huo umetolwa kupitia mahubiri ya ibada za Pasaka zilizofanyika katika makanisa tofauti nchini ikiwa ni kuadhimisha kufufuka kwa Mwokozi Yesu Kristo. Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT),
Askofu Alex Malasusa amewataka Wakristo kuenzi umoja ili kutopoteza mambo mazuri akisisitiza kuwa kila mmoja anao wajibu wa kuenzi umoja huo kwa nafasi yake.SOMA: Wakristo wasisitizwa kuishi kwa Upendo, Amani
Askofu Malasusa ametoa wito huo kupitia Ibada ya Pasaka iliyofanyika katika Kanisa la KKKT Dayosisi ya Mashariki na Pwani jana. Pia, aliwasisitiza waumini hao wasiwe watu wakuleta hofu bali wawatie moyo waliokata tamaa na kumuomba Mungu mambo yaliyokufa ndani ya maisha yaendelee kuhuishwa na kuwa mapya.
“Umoja wetu kama Wakristo, umoja wetu kama Watanzania ni vitu ambavyo tunahitaji kuvienzi lakini kuvihuisha ili mambo haya yaliyo mazuri kamwe tusiyapoteze kwa gharama yoyote na kila mmoja anawajibika katika hilo katika nafasi yake, tuyafufue na ndiyo maana ya Pasaka,” alisema.

Amesema Watanzania wamepita katika vipindi vingi vigumu lakini Mungu ameendelea kuwa pamoja nao wakati wote hadi kufikia kusherehekea sikukuu hiyo. Akizungumza katika maadhimisho ya Sikukuu ya Pasaka Kitaifa katika Kanisa Kuu la Anglikana la Mtakatifu Albano, Upanga, Dar es Salaam, Askofu Jackson Sosthenes amesema Pasaka itumike kuwapa waumini Wakikristo neema, amani na mwanzo mpya katika jamii.
Amesema kupitia Pasaka mpya Wakristo wamepokea msamaha, baraka, ujasiri na uzima wa milele, na kurejeshewa mamlaka ya kutawala na upendo. “Pasaka inakuja kwetu kutukumbusha ushindi aliotupatia Kristo msalabani ushindi ushindao hofu za ulimwengu dhidi ya dhambi na mauti kufufuka kwa Yesu kunatupatia amani katika kupatanishwa na Mungu na wengine,” alisema.
Askofu Mkuu wa Kanisa Katoliki Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Yuda Thaddaeus Ruwa’ichi ametoa wito kwa wanawake kulinda, kulea na kurithisha imani safi katika familia huku akikemea vitendo vya baadhi ya waumini kupenda kutumia mitando ya kijamii wakisahau kusaidia wenye uhitaji.
“Katika zama zetu hizi kuna vizaazaa wengi wapo watu wanataka kujibainisha kama Wakatoliki lakini si lolote, sasa ninyi mlio Wakatoliki kuweni Wakatoliki kwelikweli msiwe tia maji tia maji muwe imara thabiti na hai,” alihimiza.
![]()
Askofu wa KKKT Dayosisi ya Kaskazini Magharibi, Abednego Keshomshahara amewataka Watanzania kuendelea kuvumiliana kama njia kuu ya kudumisha mshikamano na kuleta matokeo chanya katika maisha yao ya kila siku.
“Kuna familia nyingi zimepitia mambo magumu, wamejiua kwa kukosa uvuViongozi wa dini wataka umoja, upendo, maadili, wakemea uovu milivu, kuna watu wangekuwa mbali lakini hawana uvumilivu, kama tukijifunza kuvumiliana tutapata mambo mazuri zaidi tujiepushe na kukurupuka,” alisema.
Askofu wa Jimbo Katoliki Moshi, Ludovick Minde wakati wa mahubiri katika Misa Takatifu ya Pasaka iliyofanyika katika Kanisa Kuu la Kristo Mfalme alihimiza viongozi wa kidini, wazazi na walezi kuendelea kutoa mwongozo unaofaa kwa vijana ili kuwa na taifa lenye vijana wenye maadili mema.
“Mabadiliko ya kidunia (usasa) ikiwemo ujio wa teknolojia ya kisasa pia umechangia kupungua kwa maadili mema miongoni mwa vijana tuitumie sherehe ya Pasaka ya mwaka huu kuwakumbusha kufanya kila tuwezalo ili kuokoa nafsi za vijana wetu”.
Askofu wa KKKT Dayosisi ya Magharibi, Jackson Mushendwa aliwataka waumini duniani kote kuomba na kusali ili vita vinavyoendelea maeneo mbalimbali duniani viishe. Amesema kwa sasa duniani umekuwa uwanja wa fujo ambao umesababisha madhila na maumivu makubwa kwa wanadamu.

Askofu wa Kanisa la Anglikana Dayosisi ya Central Tanganyika Dodoma, Dk Dickson Chilongani ametoa wito kwa serikali kushughulikia kero zinazowasumbua Watanzania zikiwemo za ukiritimba, kunyimwa haki na rushwa. “Unamtuma mfanyakazi ashughulikie suala muhimu anakwambia Baba Askofu tukienda wanatuomba rushwa hawaoni aibu hata kuliomba kanisa litoe rushwa, tuiombe serikali itupie macho kero hizi ili Watanzania waishi kwa furaha.”
Naye, Askofu wa KKKT Dayosisi ya Morogoro, Dk George Pindua amewasihi waumini na Watanzania kuendelea kushikamana katika upendo, kusaidiana na kuombeana mema. Aliwataka walio na uwezo wajitoe kuwasaidia walio katika uhitaji na wale wenye nguvu wawatie moyo waliokata tamaa. Askofu wa Kanisa Katoliki Jimbo la Bariadi, Prosper Lyimo amewataka waumini wa kanisa hilo kutumia sikukuu ya pasaka, kupinga vitendo vya ukatili vinavyotokea nchini.
Amesema maovu katika jamii yamekuwa mengi akiwataka Wakristo kutumia nafasi ya kufufuka kwa Yesu Kristo kukemea kwa nguvu na kupiga vita matendo yote ya ukatili wa kijinsia, pamoja na maovu ambayo yamekuwa yakitendeka katika jamii. Askofu mstaafu wa Kanisa la Anglikana Dayosisi ya Lweru, Bukoba, Jacton Rugumila amewataka waumini wa kanisa hilo kutenda haki na kujifunza kusamehe na kusahau ili waweze kusamehewa dhambi zao.
Askofu Msaidizi wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Henry Mchamungu amehubiri katika Parokia ya Mtakatifu Maximilian Maria Kolbe Mwenge, amewataka waumini wa Kikristo kuzingatia melezi bora kwa watoto ili kuwa na kizazi chenye maadili na hofu ya Mungu. Mchamungu amesisitiza kuwa malezi bora huleta watu wema kwenye jamii wenye hofu ya Mungu wasiopenda kutenda maovu.
Askofu Mkuu wa Kanisa la The Free Pentecostal Church of Tanzania (FPCT), Stivie Mulenga amewataka viongozi wa dini nchini, wakiwemo maaskofu, kutotumia majukwaa ya kidini kuchochea chuki, uchonganishi na mifarakano, badala yake wahubiri amani, upendo na mshikamano ili kulinda umoja wa kitaifa. Amesisitiza kuwa ibada zinapaswa kubaki kuwa maeneo matakatifu ya kumtukuza Mungu na si majukwaa ya kuwashambulia au kuwapendelea watu fulani kwa maslahi binafsi.
0 Comments