Mahakama Kuu ya Tanzania, Masijala Ndogo ya Dar es Salaam, imetupilia mbali maombi ya Mwenyekiti wa CHADEMA, Tundu Lissu, ya kutaka kuunganishwa katika kesi ya mgawanyo wa mali iliyofunguliwa na Makamu Mwenyekiti wa chama hicho Zanzibar, Said Issa Mohamed, pamoja na wenzake wawili. Wengine katika kesi hiyo ni Ahmed Rashid Khamis na Maulidah Anna Komu (marehemu).
Akizungumza mahakamani hapo, Wakili wa CHADEMA, Rugemeleza Nshala, amesema: “Mahakama imetoa uamuzi mdogo kuhusu maombi ya Lissu ya kuomba kuunganishwa katika kesi namba 8323 iliyoletwa na Said Issa na wenzake wawili, Ahmed Rashid na marehemu Maulidah Anna Komu, kuhusu mgawanyo wa mali. Lissu aliomba kuunganishwa, na maombi hayo yalisikilizwa na Jaji Hamidu Mwanga, ambaye alipanga kutoa uamuzi tarehe 25/03/2026.
Hata hivyo, kutokana na faili kuitwa Mahakama ya Rufaa, uamuzi huo ulisogezwa hadi leo. Uamuzi umesomwa na Msajili, ambapo mahakama imekataa kumuunganisha Lissu, ikieleza kuwa ingawa yeye ni Mwenyekiti wa chama, aliwasilisha maombi hayo kwa nafsi yake binafsi na si kwa niaba ya uenyekiti wa chama, hivyo hana maslahi ya moja kwa moja katika kesi hiyo.
Mahakama imeeleza kuwa, hata kama amri itatolewa kuhusu cheo hicho, si lazima awe yeye anayekishikilia. Hivyo, kuomba kuingia katika kesi kwa nafsi yake si sahihi, bali anaweza kushiriki kama shahidi. Kutokana na hilo, maombi yake yamekataliwa.
Aidha, kesi hiyo haipo tena kwa Jaji Hamidu Mwanga bali ipo kwa Jaji Ngunyale, ikiwa ni kesi ya msingi namba 8323. Itatajwa tena tarehe 13/05/2026 kwa ajili ya maagizo, ikiwemo kujadili iwapo kesi hiyo iliwasilishwa ndani ya muda wa kisheria wa miaka sita tangu mgogoro ulipoanza.

0 Comments