DODOMA:WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais – Mipango na Uwekezaji, Prof Kitila Mkumbo, ameweka wazi mambo sita ya msingi ambayo Taifa linapaswa kuyazingatia ili kufanikisha utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, akisisitiza matumizi ya mitaji na teknolojia, ushirikiano wa sekta ya umma na binafsi, pamoja na kujenga utamaduni wa kufanya maamuzi ya vitendo.

Akiwasilisha hotuba yake Bungeni leo, Waziri huyo amesema pamoja na Tanzania kuwa na rasilimali nyingi za asili, ni lazima ziunganishwe na mitaji na teknolojia ili ziweze kuleta tija ya kiuchumi.

Amesema Serikali itaendelea kuimarisha mazingira ya biashara na uwekezaji ili kuvutia wawekezaji wa ndani na nje ya nchi.
Katika msisitizo wake wa pili, ameeleza umuhimu wa kuimarisha ushirikiano kati ya sekta ya umma na binafsi, akibainisha kuwa mafanikio ya uchumi yanahitaji mshikamano na juhudi za pamoja kama timu moja yenye lengo la pamoja la maendeleo.

Aidha, Waziri amehimiza kujengwa kwa uthubutu wa kujaribu mambo mapya na kuachana na utegemezi wa nadharia zisizoleta matokeo, huku akisisitiza kuwa lengo kuu la uongozi ni kukuza uchumi na kuboresha maisha ya wananchi kwa vitendo vinavyoonekana.

Akihitimisha, alikumbusha kuwa maendeleo yanahitaji bidii na nidhamu ya kazi, akirejea kauli ya Hayati Julius Nyerere kuhusu umuhimu wa sera kuleta matokeo halisi kwa wananchi, na kusisitiza kuwa imani ya kumtegemea Mungu iambatane na juhudi za kazi ili kufikia maendeleo ya Taifa.