Atlético Madrid iko kwenye kiwango cha juu cha mafanikio baada ya kutinga nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa (UEFA) na wakati huo huo ikiwa na nafasi ya kunyakuwa taji la Copa del Rey mwishoni mwa wiki hii.
Timu hiyo ya kocha Diego Simeone imeonyesha ubora wake baada ya kuiondoa FC Barcelona katika hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya. Licha ya kupoteza mechi ya marudiano kwa mabao 2-1 jijini Madrid, ushindi wao wa 2-0 walioupata awali uliwapa faida ya jumla na kufanikisha safari ya kuelekea hatua ya nne bora kwa mara ya kwanza tangu mwaka 2017.
Ushindi huo umeamsha furaha kubwa kwa mashabiki wa Atletico, ambao kwa muda mrefu wamekuwa wakiishi chini ya kivuli cha wapinzani wao wakubwa, Real Madrid na Barcelona. Safari hii, Atletico wanaonekana kuwa kwenye nafasi nzuri ya kubadilisha historia hiyo.
Nahodha wa timu hiyo, Koke Resurrección, alisema ushindi dhidi ya Barcelona ni wa kihistoria na umetokana na juhudi za msimu mzima, huku akisisitiza kuwa haikuwa kazi rahisi kuifunga moja ya timu bora barani Ulaya.
Kwa upande wake, mshambuliaji Antoine Griezmann amesema mafanikio hayo ni zawadi kwa mashabiki, akiongeza kuwa timu hiyo sasa inalenga kumaliza kazi kwa kunyakuwa mataji. Atletico itashuka dimbani Jumamosi kuvaana na Real Sociedad katika fainali ya Copa del Rey itakayopigwa jijini Seville.
Atletico, ambao bado wanatafuta taji lao la kwanza la Champions League, wamewahi kufika fainali mara kadhaa bila mafanikio, ikiwemo kupoteza dhidi ya Real Madrid mwaka 2014 na 2016. Hata hivyo, matumaini yanaonekana kurejea kwa sasa huku timu ikiwa katika kiwango bora.

0 Comments