MONASTIR: TIMU ya soka ya Taifa ya Wanawake chini ya umri wa miaka 17 (Serengeti Girls), imemaliza kambi yake ya mazoezi mjini Monastir kwa sare ya bila kufungana dhidi ya wenyeji wao Tunisia kwenye Uwanja wa MustaphaBen Jannet Monastir leo.

Mechi hiyo ilikuwa ya pili kwa Serengeti Girls dhidi ya Tunisia, ya kwanza ilichezwa Machi 29 na Girls kuibuka na ushindi wa mabao 3-0.

Serengeti Girls imeweka kambi mjini Monastir nchini Tunisia kwa ajili ya maandalizi ya mechi za kufuzu fainali za kombe la dunia zilizopangwa kufanyika Morocco baadae mwaka huu.

Katika mechi ya leo, Serengeti Girls walionesha mchezo mzuri katika muda wote wa mchezo na kukosa nafasi za wazi takriban tisa katika kipindi cha kwanza.

Girls iliendelea na mashambulizi hadi kipindi cha pili lakini iliwawia vigumu kuipenya ngome ya Tunisia ambayo ilionekana kuimarika zaidi.

Baada ya mechi hiyo kesho, Serengeti Girls inatarajiwa kuanza safari ya Botswana itakapocheza mechi ya kuwania kufuzu kombe la dunia dhidi ya wenzao wa huko.

Mechi hiyo inatarajiwa kuchezwa katika Mji wa Francis town, Botswana. Endapo itaiondoa Botswana, Girls itacheza na Afrika Kusini hatua inayofuata.

Serengeti Girls imeshawahi kufuzu fainali za Kombe la Dunia mwaka 2022 zilipofanyika India na kuweka historia kwa soka la wanawake kufuzu kombe la dunia.