Mwanariadha wa Kenya Sabastian Sawe amerejea nyumbani baada ya kuwa mwanamume wa kwanza kukimbia marathon chini ya saa mbili.

Mafanikio yake ya ajabu katika mbio za London Marathon siku ya Jumapili yamepokelewa kwa fvifijo na nderemo nchini Kenya, ambapo maafisa walimkaribisha katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta jijini Nairobi.

Wazazi wake pia walikuwepo kumpokea.

Sawe alimaliza mbio hizo chini ya saa mbili kwa muda wa 01:59:30.

"Nina furaha sana, kwamba mumekuja kusherehekea nami, sikutarajia," Sawe aliuambia umati.

Wazazi wa Sawe waliendesha gari kwa saa sita kutoka nyumbani kuja kumpokea mwana wao alipotua.

Ndege ya shirika la ndege la Kenya Airways ambayo Sawe alisafiria kurejea nyumbani ilipokelewa kwa heshma maalum ilipotua, huku wacheza densi na wanamuziki wakitumbuiza.

Kurudi nyumbani kwa Sawe kulikuwa wakati wa fahari kubwa kwake binafsi, kwa familia yake, na pia kwa taifa la Kenya.