Horace Fletcher, aliyeishi mwishoni mwa karne ya 19 na mwanzoni mwa karne ya 20, alipewa jina la utani "Mtafunaji Mkuu" kwa sababu alitafuna shallot (aina ya kitunguu inayofanana na kitungu saumu) mara 722 kabla ya kuimeza.

Mtaalamu huyo wa lishe wa Marekani aliyejifundisha fani hiyo aliamini kwamba chakula kinapaswa kutafunwa hadi "kiwe laini kabisa" kiasi cha "kumezwa kwa urahisi."

Fletcher alikadiria kuwa kutafuna kabisa kungelisaidia kuokoa uchumi wa Marekani wa mwanzoni mwa karne ya 20 zaidi ya dola nusu milioni kwa siku (takriban dola milioni 19.5 za leo), kwa sababu mtu wa kawaida angetumia gramu 227 za chakula kwa siku.

Mafundisho ya Fletcher huenda yamepita kiasi, lakini "Kwa kiwango fulani alikuwa sahihi," anasema Mats Trulsson, profesa na daktari wa meno katika Taasisi ya Karolinska nchini Uswidi.

Kutafuna chakula vizuri kunaweza kuwa na manufaa kadha wa kadha, ikiwa ni pamoja na kuboresha usagaji chakula na kusababisha ulaji wa chini wa kalori, kupunguza mafadhaiko na wasiwasi, na kuboresha uwezo wa utambuzi kwa kuimarisha ustadi wa kumbukumbu na kuongeza muda wa umakini.

Kwa kuwa kuna uhusiano kati ya afya ya meno na ugonjwa wa Alzheimer na tatizo la ya kiakili, baadhi ya wataalam wanasema kuwa kuboresha afya ya meno ya wagonjwa kunaweza hata kusaidia kupunguza kasi ya kuzeeka kwa akili.

Historia ya kutafuna

Adam van Casteren, mwanabiolojia katika Taasisi ya Max Planck ya Anthropolojia ya Mageuzi huko Leipzig, Ujerumani, anasema kwamba kama wanyama wengine, wanadamu " wamekuwa na meno kwa mamilioni ya miaka." lakini, walipata mabadiliko mengi katika nyakati za kabla ya historia.

Binadamu wa kale, walioishi takriban miaka milioni sita hadi saba iliyopita, walikuwa na meno sawa na ya nyani wa kisasa.

Van Casteren anasema, "yaliwasaidia sana kula ''matunda makubwa'' ambayo yalikuwa mengi katika maeneo ya misitu ambapo babu zetu wa kale waliishi."

Kulingana na Van Casteren, mvua ilipokuza misitu mingi, makazi wazi, na hata ikolojia kama savanna, binadamu wa kale walilazimika kula "vyakula vyenye changamoto zaid kutafuna" kama vile mbegu, njugu, na mizizi.

Kwa hiyo, ni meno yao yalibadilika na kuwa mapana, makubwa, ili kukidhi ongezeko la ukubwa wa meno hayo nakubwa na nyuso ili kushughulikia meno haya yote, pamoja na misuli kubwa inayohitajika kuziendesha.

Meno hayo yaliwawezesha kusaga,chakula kabla hakijamezwa ili kiwe rahisi kwa usagaji wa tumbo.

Van Casteren anasisitiza kwamba ukuaji wa teknolojia, usindikaji wa chakula, na kilimo, pamoja na moto wa kupikia chakula, hitaji letu la kutafuna kwa muda mrefu limepungua sana kama haujatoweka. Leo, wanadamu hutafuna kwa takriban dakika 35 kwa siku, huku sokwe na bonobos, hutafuna kwa saa 4.5, na sokwe na orangutan hutafuna kwa saa 6.6.

Licha ya mabadiliko haya ya kimageuzi, madhumuni ya kutafuna bado ni sawa.

Van Casteren anasema, "Sisi mamalia ni watafunaji wagumu sana kwa sababu tunataka kupata nishati nyingi iwezekanavyo kutoka kwa chakula chetu ili kuchochea joto na damu mwilini."

Kutafuna kunasaidia kunameng'enya chakula katika vipande vidogo na kuvilowesha kwa mate, na hivyo kuvimeza kwa urahisi.

Andries van der Bilt, mtaalamu wa fiziolojia ya mdomo na kutafuna ambaye alifanya kazi kama mtafiti katika Kituo cha Matibabu cha Chuo Kikuu cha Utrecht nchini Uholanzi kwa zaidi ya miaka 30, anasema, "Hii ni hatua ya kwanza ya usagaji chakula."

Trulsson anasema, ''usipotafuna, utumbo wako hauko tayari kuchakata chakula."

Abhishek Kumar, mwanasayansi wa magonjwa ya mfumo wa neva ambaye anafanya kazi na Trulsson katika Taasisi ya Karolinska, anasema kwamba kitendo cha kumeng'enya chakula katika vipande vidogo pia huongeza eneo lao la uso, kumaanisha kuwa maji ya usagaji chakula yanaweza kuvifanyia kazi kwa ufanisi zaidi.

Hii ni muhimu kwa afya ya utumbo.

Chembe kubwa zaidi huwa zinabaki ndani ya utumbo kwa muda mrefu, hivyo basi huwapa vijidudu muda zaidi wa kuzichachisha.

Kulingana na Kumar, hii husababisha "bloating, hisia ya ukamilifu, kuvimbiwa, na dalili nyingine."

Inaimarisha ufyonzaji wa virutubishi na kujihisi kushiba

Kutafuna husaidia mwili kufyonza virutubishi kutoka kwa chakula, na hivyo kuimarisha afya.

Kwa mfano, katika utafiti wa 2009, watu wazima 13 wenye afya nzuri waliagizwa kutafuna lozi chache mara 10, 25, au 40.

Watafiti walipokusanya sampuli za kinyesi kutoka kwa washiriki, waligundua kuwa kadiri watu walivyotafuna ndivyo mafuta yanavyopungua. Hii inaonyesha kuwa unyonyaji wa nishati kutoka kwa mlozi ulikuwa karibu theluthi moja juu.

Zaidi ya hayo, kutafuna mara 40 kuliwasaidia washiriki kujihisi kushiba kwa muda mrefu. Utafiti tofauti wa 2013 pia uliunga mkono kiungo hiki cha shibe.

Hii ni kwa sababu inachukua kama dakika 20 kwa mwili kudhibiti uzalishwaji wa homoni zinazohusiana na njaa na kutuma ishara kwa ubongo kuujulisha kuwa umeshiba. Kutafuna pia hukupa muda zaidi.

Kwa hiyo, wataalamu wengi wa chakula na madaktari wanatetea kula polepole na kwa uangalifu, badala ya kumeza chakula haraka, hasa ikiwa unajaribu kupoteza uzito.

Utafiti wa watoto 92 nchini Brazil uligundua kuwa watoto wanene "walitafuna kidogo na kula haraka" ikilinganishwa na watoto walio na uzani wa kawaida.

Kwa kweli, njia nzuri ya kupunguza kasi ya kula ni kula vyakula ambavyo sio rahisi kutafuna haraka.

Tafiti nyingi zinapendekeza kuchagua vyakula kigumu badala ya vile ambavyo vinalika kwa urahisi (kama machungwa badala ya maji ya machungwa) na vyakula vyenye mnato mwingi badala ya vyakula vyenye mnato mdogo (kama vile oatmeal na mbegu za lin badala ya wali mweupe au pasta).

Kumar anasema, "Muundo wa chakula unaweza kuathiri jinsi tunavyoshiba, na kwa hivyo inaweza kusaidia wale wanaopambana na unene kupunguza uzito kwa kupunguza ulaji wao wa chakula."

Kando na lishe na usagaji chakula, watafiti wanagundua kuwa kutafuna kunachukua jukumu muhimu katika nyanja zingine za maisha tunapozeeka, haswa afya ya ubongo.

Kumar anasema, "Kuna shauku inayoongezeka katika 'mhimili wa kuumwa na ubongo,' ambao unapendekeza uhusiano wa moja kwa moja kati ya kutafuna na afya ya ubongo."

Kwa mfano, kupoteza jino pia kunahusishwa na hatari ya kuongezeka kwa ugonjwa wa Alzheimer na shida ya akili.

Kumbukumbu pia huathiriwa. Katika utafiti uliohusisha zaidi ya watu 28,500 walio na umri wa zaidi ya miaka 50 katika nchi 14 za Ulaya, washiriki ambao walikuwa na uwezo mzuri wa kutafuna au ambao hawakutumia meno bandia walifanya vyema katika majaribio mbalimbali ya utambuzi.

Ikilinganishwa na wale walio na matatizo ya kutafuna, walifanya vizuri zaidi katika kukumbuka maneno, ufasaha wa maongezi, na ustadi wa kuhesabu.

Katika uchunguzi wa watu 273 wenye afya wenye umri kati ya miaka 55 na 80, wanasayansi waligundua kwamba wale ambao walihifadhi zaidi meno yao ya asili walikuwa na kumbukumbu bora ya semantic na ya muda mrefu.

Kutafuna kunahusiana vipi na kumbukumbu?

Watafiti wengine wanahusisha hili na mizunguko ya neva inayounganisha kiungo chetu cha kutafuna na hipokampasi (eneo la ubongo linalohusika na kujifunza na kuhifandhi kumbukumbu mpya; mojawapo ya maeneo ya kwanza yanayoathiriwa na Alzeima).

Wengine wanasema kwamba kutafuna vitu vyenye vigumu na laini kunaweza kuongeza mtiririko wa damu kwenye ubongo, kama walivyobaini watafiti wa Japan katika majaribio la utafunaji wa ubani.

Trulsson anaeleza, "Kulingana na nadharia, kutafuna hufanya kama pampu inayotuma damu kwenye ubongo." Anasema hii hufanya ubongo kuwa makini na kufanya kazi vizuri.

Ili kubaini kama kutafuna vibaya husababisha kudorora kwa utambuzi, timu ya Trulsson kwa sasa inafanya jaribio ambalo hubadilisha meno ya wagonjwa yaliyong'oka kwa vipandikizi na kuchunguza utendakazi wa ubongo kabla ya upasuaji na kwa hadi mwaka mmoja baadaye.

Uchunguzi wa ubongo wa MRI pia utatumika kuchunguza kama "White Matter'' inafanya kazi kama nyaya zinazounganisha na kuruhusu maeneo tofauti ya ubongo kuwasiliana na kuongea na mwili. Lesions au madoa haya hutokea pale ambapo nyuzi hizi za neva zinapoharibika au kupoteza ulinzi wake.

Hiki ni kiashirio cha kuharibika kwa afya ya mishipa ya ubongo, hupungua kwa matibabu.

Inaongeza umakini

Baadhi ya tafiti zimegundua kwamba kutafuna ubani pia kunaimarisha umakini miongoni mwa watu.

Utafiti wa uchanganuzi wa data uliojumuisha watu 21 uligundua kuwa washiriki waliotafuna tambi wakati wa wakifanya kazi zenye changamoto ya utambuzi walikuwa naumakini ikilinganishwa na wale ambao hawakutafuna ubani. Ni vyema kutambua kwamba utafiti huu ulifadhiliwa na mtengenezaji wa ubani wa Mars Wrigley.

Utafiti huru wa washiriki 80 pia uligundua kuwa kutafuna ubani kuliboresha viwango vya tahadhari kwa 10% wakati mtu anapofanya mfululizo wa kazi za utambuzi. Wale waliotafuna ubani pia walifanya vizuri zaidi kwenye jaribio la kijasusi.

Wanasayansi "hawajabaini jinsi mchakato huo unavyofanya kazi," Trulsson anasema, "Kiungo kati ya kutafuna na kuongezeka kwa umakini ni nguvu sana."

Hata hivyo, kuna caveat. "Athari labda haitadumu zaidi ya dakika 15 hadi 20," lakini wataalam hawajui ni kwa nini.

Katika jaribio lingine, vijana walioombwa kufanya kazi nne za kompyuta kwa wakati mmoja huku wakitafuna ubani na wenngine waliambiwa kufanya vivyo hivyo bila kutafuna ubani na matokeo yalionyesha wale waliokuwa wakitafuna ubani walikuwa makini zaidi kwa 20% .

CH akushangaza ni kuwa ufanisi huo uliambatana na kupungua kwa wasiwasi, dhiki, na viwango vya cortisol (kiashiria cha kawaida cha kibayolojia cha dhiki).

Inapunguza msongo wa mawazo

Kutafuna husaidia kukabiliana na msongo wa mawazo hata nje ya maabara.

Kundi la watafiti wa Kituruki, walifanya utafiti uliojumuisha wauguzi 100 waliokuwa wakijiandaa kwa mtihani wa katikati ya muhula. Watafiti hao walibaini kuwa wauguzi waliotafuna ubani kwa walau dakika 30 kwa siku walikua na viwango vya chini vya wasiwasi unaotokana na msongo wa mawazo.

Jianshe Chen, mtafiti katika Mamlaka ya Sayansi, Teknolojia na Utafiti ya Singapore, anasema kuwa kutafuna kunaonekana kuwa jambo la kawaida miongoni mwa watahiniwa:

"Baadhi yao huanza kusaga meno bila kujua wanapokuwa na msongo wa mawazo."

Ugonjwa wa Bruxism, au kusaga meno, ambao hutumia misuli ya taya sawa na kutafuna na huathiri mtu mmoja kati ya kumi, mara nyingi huchochewa na mfadhaiko na wasiwasi.