DODOMA; WAZIRI wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mahmoud Thabit Kombo, amesema  Tanzania inaendelea kudumisha misingi ya uhusiano na ushirikiano na msimamo wake ni uleule wa kutofungamana na upande wowote.

Balozi Kombo ametoa kauli hiyo bungeni leo Mei 26, 2026 alipokuwa akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya wizara hiyo kwa Mwaka wa  Fedha 2026/27.

“Tanzania imeendelea kudumisha misingi ya uhusiano na ushirikiano wa kimataifa, kama ilivyowekwa na waasisi wa Taifa letu na kama ilivyoainishwa katika Sera ya Mambo ya Nje ya Mwaka 2001, Toleo la 2024.

“Misingi hiyo ni Kulinda Mamlaka kamili ya nchi, mipaka ya nchi na uhuru wa kisiasa wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania; Kulinda uhuru, haki za binadamu, usawa na demokrasia; Kukuza ujirani mwema na Kukuza Umoja wa Afrika.

“Mheshimiwa Spika, misingi mingine ni kuongeza ushirikiano wa kiuchumi na washirika wa maendeleo; kuwezesha utekelezaji wa sera ya kutofungamana na upande wowote na ushirikiano wa nchi zinazoendelea; kuunga mkono Umoja wa Mataifa katika kuimarisha maendeleo ya kiuchumi, amani na usalama; na kulinda maadili, mila, desturi na utamaduni wa watu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

-Misingi hii imechangia kudumisha heshima na taswira njema ya Taifa letu kupitia ushirikiano wa uwili, kikanda na kimataifa,” amesema Waziri Kombo