
DAR ES SALAAM: MKURUGENZI Mkuu wa Tume ya TEHAMA, Dk Nkundwe Mwasaga, amesema uchumi wa kidijitali wa Tanzania unaendelea kukua kwa kasi na kuvutia wawekezaji kutoka mataifa mbalimbali duniani. Amesema Tume ya TEHAMA inaendelea na jukumu la kusajili kampuni changa pamoja na kampuni za TEHAMA, sambamba na kuhamasisha uwekezaji katika sekta hiyo.
Ameeleza kuwa kuna tofauti ya msingi kati ya e-government na e-governance, akifafanua kuwa e-governance inahusisha usimamizi wa sekta nzima ya nchi kwa njia ya kidijitali. Amebainisha kuwa mfumo huo unajumuisha sekta ya umma, sekta binafsi, kampuni changa za teknolojia na wadau wengine wa uchumi wa kidijitali.
Akizungumza jijini Dar es Salaam katika warsha iliyoandaliwa kwa ushirikiano wa HSE University, Serikali ya Urusi, Tume ya TEHAMA Tanzania na Umoja wa Mataifa, amesema tukio hilo ni ushahidi kuwa Tanzania inaendelea kuwa kivutio kikubwa katika uchumi wa kidijitali.
Ameongeza kuwa kampuni nyingi za kimataifa zimeonesha nia ya kuingia katika soko la Tanzania, akibainisha kuwa nafasi ya kimkakati ya nchi katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kusini mwa Afrika inaiweka Tanzania katika nafasi muhimu ndani ya miundombinu ya kidijitali ya kimataifa.
Dk Mwasaga amesema Tanzania imeendelea kuvutia kampuni mbalimbali kutoka Urusi ambazo zimeonesha nia ya kushirikiana na kampuni za ndani katika uwekezaji wa teknolojia tofauti. Amesema ushirikiano huo unatarajiwa kuwa na manufaa kwa pande zote mbili.
Amefafanua kuwa Serikali inaendelea kuboresha mazingira ya utawala wa kidijitali kupitia ripoti mpya inayozinduliwa, ambayo inaonesha mafanikio yaliyofikiwa pamoja na maeneo yanayohitaji maboresho katika mfumo wa digital governance nchini.

Aidha, amesema Tanzania inaendelea kuvutia uwekezaji katika miundombinu ya mawasiliano, ikiwemo nyaya za chini ya bahari na ujenzi wa vituo vya kuhifadhi data (data centres). Amesema baadhi ya kampuni za kimataifa zinafikiria kuhamishia shughuli zao nchini kutokana na mazingira mazuri ya uwekezaji.
Kuhusu kampuni changa, Dk Mwasaga amesema Tume ya TEHAMA inazisajili katika makundi matatu ya silver, gold na tanzanite, ambapo kampuni za tanzanite zina uwezo wa kushindana katika soko la kimataifa na kuwakilisha Tanzania nje ya nchi.
Amesema warsha hiyo imefungua fursa kwa kampuni changa za Tanzania kushirikiana na wenzao kutoka Urusi kwa ajili ya kubadilishana uzoefu na teknolojia, akisisitiza kuwa utawala wa kidijitali nchini unaendelea kukua na ni sehemu muhimu ya utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
Kwa upande wake, Mratibu wa programu ya Urusi ya utawala wa kidijitali Afrika, Andrey Maslov, amesema Tanzania ina nafasi kubwa ya kutumia mifumo ya kidijitali kuharakisha maendeleo ya kiuchumi na kufikia malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
Amesema programu hiyo inalenga kuhamisha na kushirikisha uzoefu wa kimataifa katika utawala wa kidijitali kwa nchi za Afrika, ili kusaidia mageuzi ya kiuchumi na kijamii kupitia teknolojia.
Maslov amesema tukio hilo limekuja kwa wakati sahihi, akibainisha kuwa uzoefu wa Urusi na nchi nyingine unaweza kusaidia kuimarisha ushirikiano kati ya taasisi za Urusi, Tanzania na mataifa mengine ya Afrika yanayoshiriki programu hiyo.

Akizungumzia Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 inayotarajiwa kuzinduliwa Julai mwaka huu, amesema inaonesha dhamira ya serikali kutumia teknolojia kama chombo kikuu cha mageuzi ya maendeleo ya kiuchumi na kijamii.
Ameeleza kuwa mifumo ya kidijitali itasaidia kuongeza ufanisi wa huduma za serikali, kuharakisha maendeleo na kufanikisha lengo la kufikia uchumi wa dola trilioni moja ifikapo mwaka 2050.
Hata hivyo, Maslov amebainisha kuwa utekelezaji wa utawala wa kidijitali unakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo usalama wa mtandao, uhifadhi wa taarifa na upungufu wa wataalamu wa teknolojia.
Amesema usalama wa kidijitali sasa unaathiri sekta zote muhimu zikiwemo chakula, nishati na uchumi, hivyo akasisitiza umuhimu wa nchi kuwekeza katika mifumo madhubuti ya ukusanyaji, uchakataji na ulinzi wa data ili kulinda maendeleo ya taifa.
0 Comments