
DAR ES SALAAM: Kongamano maalumu lililowakutanisha wanawake kutoka sekta mbalimbali limefanyika ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Siku ya Mama Duniani, kwa lengo la kujadili na kujifunza masuala mbalimbali yanayohusu maendeleo ya familia, malezi pamoja na ukuaji wa uchumi kwa wanawake.

Akizungumza katika kongamano hilo lililofanyika Dar es salaam, Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Dar es Salaam Bona Kamoli amewahimiza wanawake kutumia fursa ya mikopo ya asilimia 10 inayotolewa na halmashauri ili kujikwamua kiuchumi na kuboresha maisha ya familia zao.
Amesema wanawake wanapaswa kuwa mstari wa mbele katika shughuli za maendeleo kwa kutumia fursa zilizopo kujiongezea kipato.

Aidha, washiriki wa kongamano hilo walijadili umuhimu wa kujenga familia zenye maadili mema, kuimarisha malezi ya watoto pamoja na kukuza uwezo wa wanawake katika shughuli za kiuchumi kwa manufaa ya jamii.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Thamani Yangu Foundation amesema wazazi wanapaswa kuweka msingi mzuri wa malezi kwa watoto wao tangu wakiwa wadogo, ili kuwajengea maadili na misingi imara itakayowasaidia kuwa raia wema katika jamii.
0 Comments