MOROGORO: Asasi za kiraia zimetakiwa kuwasilisha mapendekezo yatakayosaidia kutatua changamoto zinazoendelea kukwamisha utekelezaji wa majukumu ya Serikali, hususan katika kuhakikisha kila Mtanzania anafurahia kikamilifu haki zake za msingi za binadamu.

Wito huo umetolewa na Wakili wa Serikali Mfawidhi Mkoa wa Morogoro, Xevia Masalu, aliyemwakilisha Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria, wakati wa kikao kazi kilichowakutanisha wadau mbalimbali wa asasi za kiraia, wakiwemo watetezi wa haki za binadamu, wanawake na watu wenye ulemavu.

Kikao hicho kimelenga kuhakiki na kuthibitisha rasimu ya taarifa kuhusu hali ya haki za binadamu nchini, kwa lengo la kuhakikisha kuwa taarifa hiyo inakuwa jumuishi, sahihi na inayoakisi uhalisia wa changamoto zilizopo katika jamii.

Aidha, Masalu amebainisha kuwa Serikali imekuwa ikishiriki kikamilifu katika mchakato wa Universal Periodic Review (UPR) tangu kuanzishwa kwake, ikiwa ni sehemu ya jitihada endelevu za kuimarisha na kuboresha mifumo ya haki za binadamu nchini.

Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Haki za Binadamu katika Wizara ya Katiba na Sheria, Hadija Kissa, amesema kuwa jukumu la Serikali ni kulinda, kukuza na kuendeleza haki za binadamu. Ameongeza kuwa maandalizi ya taarifa hiyo ni uthibitisho wa dhamira ya Tanzania katika kutekeleza kwa vitendo wajibu huo.