
ARUSHA: Serikali imeagiza waajiri na wasimamizi wa rasilimali watu nchini kuhakikisha watumishi wote wenye sifa na waliotengewa bajeti ya kupandishwa vvyeo Mei mwaka huu wanapandishwa vyeo bila kuwapo kwa ucheleweshaji wowote.

Agizo hilo linasisitiza kukamilika kwa taratibu zote za kisheria na kanuni kwa wakati, huku serikali ikionya kuwa haitavumilia malalamiko ya watumishi ambao haki zao zinakwama kutokana na uzembe wa maafisa utawala.

Hayo yamesemwa leo jijini Arusha na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Ridhiwani Kikwete, wakati akifungua mkutano wa pili wa Jumuiya za Wataalamu wa Utawala na Rasilimaliwatu (AAPAM Tawi la Tanzania) jijini Arusha.

Amebainisha kuwa ofisi yake haitegemei kupokea malalamiko ya watumishi walioachwa wenye sifa huku akisisitiza kuwa watumishi waliojiendeleza lazima wabadilishiwe kada kulingana na miongozo iliyowekwa, kwani kufanya kinyume ni kutowajibika ipasavyo.

Katika hatua nyingine, Waziri Kikwete ameagiza mabadiliko makubwa ya utendaji kazi ndani ya utumishi wa umma, akisisitiza kuwa kuanzia sasa maafisa rasilimaliwatu na utawala nchini lazima wahakikishe wanajenga usalama wa kisaikolojia kwa watumishi.
0 Comments