KAMATI ya Kudumu ya Bunge Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) imempongeza Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, kwa ujenzi wa  shule za kisasa za ghorofa  wilayani Ilala na kueleza kwa mara ya kwanza kamat hiyo imeshuhudia  jengo la shule ya sekondari ya kata yenye lifti.

Hayo yameelezwa na Mwenyekiti wa kamati hiyo  Florent Kyombo, katika ziara ya wajumbe wa kamati hiyo kukagua miradi  ya maendeleo katika Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaa, hususan ujenzi  wa  Shule ya  Sekondari ya Bonyokwa  itakayo chukua wanafunzi wa kidato cha tano na sita.

Kyombo amesema  kamati yake imezunguka mikoa mingi Tanzania lakini haijawahi kukutana na  jengo la shule lenye  hadhi  kama hilo la Shule ya Sekondari Bonyokwa lenye lifti.

"Jiji la Dar es Salaam wameupiga mwingi. Msione vinaelea viumeundwa. Tumezunguka mikoa mingi lakini hatujakutana na jengo lenye hadhi kama hii,"ameeleza  Mbunge Kyombo.

Amesema  kamati hiyo inamshukuru Rais Dk. Samia, kwa uwekezaji mkubwa katika sekta ya elimu hususan ujenzi wa shule za ghorofa ambao utaondoa adha kwa wanafunzi.

"Kamati inawaomba wanafunzi kumlipa Rais Dk. Samia, kwa kufanya vizuri  darasani na  kutunza mundombinu hii,"amebainisha  Kyombo.

Ameongeza  licha ya kutembelea na kukagua jengo hilo  la shule lakini maelezo ya awali  ya viongozi wa wilaya ya Ilala na Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam yanadhihirisha ujenzi  wa majengo mengi ya ghorofa hivyo kupongeza viongozi kwa utekelezaji wa miradi hiyo .

Hata hivyo kamati hiyo ilielekeza  halmashauri hiyo kuboresha majengo ya Shule ya Msingi Bonyokwa na Shule ya Sekondari Bonyokwa ya kiadato cha kwanza na cha nne, yawiane kidogo na hadhi ya jengo hilo la kissa.

Mbali na mradi huo, kamati hiyo mekagua  ujenzi wa Barabara ya Kwa mpalange (Buza) Temeke-Kitunda unaogharimu  kilometa 6.2, ujenzi wa Kituo cha Afya Mchikichini unaotekelezwa katika Kata ya Mchikichini unaogharimu sh. bilioni 7.4.

Awali Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo, alimshukuru Rais Dk. Samia, kwa kuelekeza fedha nyingi za miradi wilayani humo na kwamba wataendelea  kusimamia kikamilifu kuhakikisha miradi hiyo inakamilika kwa wakati

Mpogolo, ameeleza  ujenzi wa shule za ghorofa ni mkakati uliwekwa kuelekea utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo  2050 na kusimamia maono ya Rais Dk. Samia, wanafunzi wanasoma katika mazingira rafiki.

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam,Elihuruma  Mabelya,  amesema  katika mwaka wa fedha 2026-27  wametenga sh. bilioni 19 kuboresha mundombinu ya elimu.

Mabelya amesema   mradi wa ujenzi wa Shule ya Sekondari Bonyokwa  umegharimu sh. bilioni 2.07  na ina madarasa 20, matundu ya vyoo 45 yakijumuisha matundu ya vyoo vya kawaida 30, matundu ya watu wennye mahitaji maalum 10, sehemu za  kujisaidia haja ndogo tano kwa wavulana, vyumba vitano  maaluma kwa wasichana vyenye choo ndani yake

"Shule hii inatarajia kuchukua wanafunzi 1400 mwaka 2026/27 na mwaka  mwaka 2028  shule  itachukua wanafunzi 3100,"amesema Mabelya.

Mbali na jengo la Shule ya Sekondari Bonyokwa kuwa na lifti  shule nyingine  ambayo jengo lake lina lifti wilayani humo ni Shule ya Sekondari  Kipunguni B.